IQNA

Kiongozi wa Hizbullah aapa utii kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

15:33 - March 12, 2026
Habari ID: 3482049
IQNA – Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem, katika ujumbe wake amempongeza Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei na kuapa utiifu kwake.

 

Katika ujumbe wake, Kiongozi wa Hizbullah amesema: “Kwa furaha na fahari kubwa tulipokea habari ya kuchaguliwa kwako kwa haki na kwa ustahiki na Baraza la Wanazuoni Wataalamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa Kiongozi na Marjaʿ (mwanazuoni mwenye mamlaka kufuatwa katika madhehebu ya Shia ), mrithi aliyebarikiwa na mwaminifu katika kulinda njia ya Imam Khomeini (RA), njia ambayo Imam Khamenei (RA) aliitolea maisha yake ya thamani pamoja na damu ya mashahidi waaminifu ili kuhifadhi uhuru wa Iran na utambulisho wake halisi wa Mtume Muhammad (SAW),”

“Katika Hizbullah ya Lebanon, huku tukimshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema zake nyingi zilizowezesha maendeleo yetu ya kisiasa, kimaadili na kimapinduzi,  muqawama thabiti uliopata msukumo kutoka Mapinduzi ya Kiislamu yenye baraka ya Iran na kutoka katika harakati ya ukombozi na kujitegemea, chini ya uongozi wa Sayyid Abbas al‑Musawi, Sayyid Hassan Nasrallah, na Sayyid Hashem Safieddine (Mwenyezi Mungu awaridhie) , tunatoa pongezi zetu za dhati kwa kuchaguliwa kwako kwa ustahiki.”

Sheikh Naim Qassem ameongeza: “Tunathibitisha kwamba kama tulivyoapa utiifu kwa kiongozi wetu shahidi na mlezi wetu, Imam Khamenei, pamoja na Imam wetu mwanzilishi, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awaridhie wote wawili), tunaendelea kusimama imara katika ahadi yetu kwa uongozi wako, kwa ajili ya kuitumikia dini, haki na ubinadamu, na kuandaa mazingira ya kudhihiri kwa uadilifu kupitia baraka za Bwana wa Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).”

Amemalizia kwa kusema: “Kwa niaba yangu na ndugu zangu katika Baraza la Hizbullah pamoja na makamanda na Mujahidin wa Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon, tunatangaza upya ahadi yetu ya utii kwako na tunamuomba Mwenyezi Mungu akujalie mafanikio katika kutimiza matarajio ya taifa lako na ya watu wote waliodhulumiwa, ili kuwaweka huru wao na ardhi zao kutokana na madhara ya madhalimu na wanyanyasaji.”

Baada ya kuuawa shahidi kwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika shambulio la Marekani na Israel tarehe 10 Ramadhani sawa na 28 Februari, Baraza la Wataalamu la Iran tarehe 8 Machi 2026 lilimchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

4340044

captcha