IQNA

Eid al‑Fitr Huleta Wapendwa Pamoja Duniani Kote

15:04 - March 20, 2026
Habari ID: 3482075
IQNA – Baada ya kuonekana au kutokuonekana kwa hilali ya mwezi wa Shawwal katika mabara mbalimbali, Waislamu duniani wanaadhimisha Eid al‑Fitr katika siku tofauti.

Waislamu kote ulimwenguni wanaaga mwezi mtukufu wa Ramadhani na mwaka huu wengine wameadhimisha sikukuu ya Eid al‑Fitr leo Ijumaa  20 Machi na wengine kesho Jumamosi 21 Machi.

Kwa kawaida Eid hupokelewa kwa furaha na shangwe, na huadhimishwa kwa swala za jamaa, sherehe mbalimbali, kutembeleana na familia, mikusanyiko ya kijamii, matembezi pamoja na kuvaa nguo mpya.

Hata hivyo mwaka huu, Eid inakaribia huku kukiwa na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, hali ambayo imezua wasiwasi katika nchi nyingi za Mashariki ya Kati na kuleta athari pana hata nje ya eneo hilo.

Nchini Marekani, Waislamu wengi waliadhimisha mila za kidini na kijamii za Ramadhani mwaka huu wakiwa katika mazingira ya matukio ya ndani na ya kimataifa yanayozua wasiwasi. Haya ni pamoja na hofu kuhusu hatua kali za sera za uhamiaji, matamshi yanayochochea chuki dhidi ya Waislamu, pamoja na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati ambako wengi wana ndugu na jamaa.

Eid al‑Fitr ni sikukuu ya Kiislamu inayoadhimisha mwisho wa mwezi wa Ramadhani, kipindi ambacho Waislamu wanaofunga hufunga kila siku kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua. Ramadhani ni wakati wa kuongeza ibada, kutoa sadaka na kufanya matendo mema, na mara nyingi huambatana na mikusanyiko ya furaha wakati wa kufuturu.

Neno Eid al‑Fitr linamaanisha sikukuu ya kufungua au kuvunja saumu.

Uislamu hutumia kalenda ya mwezi, hivyo Ramadhani na Eid hubadilika katika misimu mbalimbali kila mwaka.

Kwa kumtakia mtu anayesherehekea Eid, unaweza kusema “Eid Mubarak,” yaani Eid yenye baraka na furaha.

Nchini Indonesia, watu wengi husafiri kurejea katika miji au vijiji vyao vya asili ili kusherehekea sikukuu pamoja na familia zao katika utamaduni wa kurejea nyumbani. Kabla ya sikukuu, masoko huwa na shughuli nyingi huku watu wakinunua nguo, viatu, biskuti na peremende.

Nchini Malaysia, Waislamu pia wana utamaduni wa kurejea nyumbani wakati wa Eid. Siku ya kwanza kwa kawaida huanza kwa swala ya asubuhi msikitini, kisha watu huombana msamaha na kutembelea makaburi ya wapendwa wao.

Kuna pia utamaduni wa “open house”, ambapo marafiki na familia hutembeleana kusherehekea Eid na kufurahia vyakula vya jadi. Wazee huwapa watoto na wageni zawadi ya fedha katika bahasha za kijani.

Nchini Misri, familia hushiriki swala ya Eid katika mazingira ya shangwe. Wengi hutembelea ndugu, marafiki au majirani, na wengine husafiri kwenda maeneo ya mapumziko. Watoto, mara nyingi wakiwa wamevaa mavazi mapya ya Eid, hupokea zawadi ya fedha inayojulikana kama “eidiya.”

Kutengeneza au kununua biskuti za Eid zilizosheheni sukari ya unga pia ni sehemu muhimu ya maadhimisho ya sikukuu hiyo nchini humo.

Nchini Marekani, ambako Waislamu ni jamii ndogo yenye asili na tamaduni mbalimbali, wengi hukusanyika kwa swala ya Eid na sherehe za familia zenye shughuli za burudani kwa watoto, kama vile kupaka rangi usoni na michezo ya maputo.

3496824/

captcha