IQNA

Maelezo ya Mradi wa 4 wa Qur’ani wa Al‑Azhar

14:13 - May 15, 2026
Habari ID: 3482240
IQNA – Kituo cha Kiislamu cha Al‑Azhar nchini Misri kimeatangaza kuanza kwa msimu wa nne wa mradi wa majira ya joto wa Qur’ani unaolenga kuhudumia Kitabu Kitukufu na kufundisha Neno la Wahyi kwa njia ya malezi ya kiroho.

Mradi huu utafanyika kuanzia Juni 1 hadi Agosti 31, 2026, chini ya usimamizi wa Sheikh Ahmad Al‑Tayeb, Sheikhe Mkuu wa Al‑Azhar.

Mwaka huu mradi unatoa mfumo wa kina wa programu za kielimu na za Qur’ani kwa makundi mbalimbali ya umri, ukichanganya kuhifadhi, kufasiri, na kutafakari Qur’ani sambamba na kufufua Sunnah ya Mtume Muhammad (SAW) , yote yakijumuishwa katika upeo mpana wa elimu ya kiroho na kijamii.

Shabaha kuu ni kuimarisha uhusiano wa vijana na Qur’ani Tukufu pamoja na Sunnah ya Mtume Mtukufu (SAW).

Mradi huu wa majira ya joto unatekelezwa kwa mwaka wa nne mfululizo, baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika misimu iliyopita ambapo wanafunzi na wazazi walishiriki kwa wingi.

Kutokana na utekelezaji wake mzuri na mapokeo makubwa kutoka kwa wananchi wa Misri, Al‑Azhar imelitaja kuwa mojawapo ya miradi yake mashuhuri zaidi ya kusambaza elimu ya Qur’ani na kujenga misingi ya Uislamu wa wastani.

Vipengele vikuu vya mradi

1.   Mpango wa “Wahifadhi Qur’ani 10,000” ,  ukilenga kuhitimu wahifadhi 10,000 wa Qur’ani nzima, kupitia zaidi ya vituo 12,000 vya binafsi vya kuhifadhi Qur’ani chini ya usimamizi wa Al‑Azhar kote nchini Misri.

2.   Programu ya “Hifadhi Mtaala Wako”, iliyoandaliwa mahsusi kwa wanafunzi wa taasisi za Al‑Azhar.

Inafanyika mara tatu kwa wiki na inalenga kuwasaidia wanafunzi kuhifadhi mtaala wa mwaka wa masomo ujao, ili kutumia likizo ya majira ya joto ipasavyo na kupunguza mzigo wa masomo katika mwaka mpya.

3.   Jukwaa la Qur’ani Tukufu, mfumo wa mtandaoni unaotoa huduma za kuhifadhi Qur’ani kwa mbali kwa wanafunzi wa Al‑Azhar na watakaotaka kuhifadhi Qur’ani kipindi cha majira ya joto.

Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa Al‑Azhar wa kutumia zana za kidijitali katika elimu ya Qur’ani na kupanua wigo wa ushiriki wa kielimu miongoni mwa Waislamu.

4.   Kufufua Sunnah ya Mtume (SAW) , kupitia vipindi vya kusoma na kusikiliza Hadithi za Mtume katika vituo na taasisi za kuhifadhi Qur’ani vya Al‑Azhar, ili kuleta mapenzi na uelewa wa kina wa urithi wa Mtume katika nyoyo za wanafunzi.

Aidha, mradi huu unahusisha sherehe za Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Qur’ani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Agosti.

Katika shughuli hizo, hushuhudiwa usomaji wa Qur’ani yote kwa siku moja au sehemu zake, ambapo mwaka uliopita zaidi ya washiriki 100,000 walihudhuria kutoka ndani ya Misri pamoja na maelfu kutoka mataifa mengine.

 3497456

Habari zinazohusiana
Kishikizo: al azhar qurani tukufu
captcha