IQNA

Mtazamo

Lango Bahari La Hormuz na mapambano ya kudhibiti mfumo wa usalama na utambulisho wa Asia Magharibi

10:22 - July 27, 2026
Habari ID: 3482543
Hormuz
IQNA – Mchambuzi wa kisiasa kutoka Lebanon anaamini kuwa mvutano unaoendelea katika Lango Bahari La Hormuz si mapambano ya kawaida juu ya njia ya majini, bali ni vita vikali vya kuamua hatima na utambulisho wa mfumo wa kiusalama katika eneo la Asia Magharibi.

Ndugu Jihad Haidar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Lebanon, amechapisha makala kupitia tovuti ya habari ya Al-Ahed. Uchambuzi wake ni kama ifuatavyo:

Mzozo wa Lango Bahari La Hormuz hivi leo hauhusu tu uhuru wa upitishaji wa vyombo vya baharini au usalama wa nishati; bali ni harakati za kupanga upya mizani ya nguvu katika Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi. Lango hilo sasa limekuwa chombo muhimu cha kisiasa kinachotumiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelezea upya kanuni za uzuiaji (deterrence) na ushawishi wa kikanda. Kwa upande mwingine, Marekani inaona kuwa kuzuia maendeleo haya ni jambo la dharura ili kulinda mfumo wa kikanda unaozingatia maslahi yake na ya washirika wake, hususan utawala haramu wa Kizayuni. Hivyo basi, athari za mzozo huu zinavuka mipaka ya uchumi wa kimataifa na kugusa moja kwa moja usalama wa ndani wa utawala huo unaokalia ardhi za eneo kwa mabavu.

Iran inatambua vyema kuwa mizani ya kijadi ya kijeshi dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni haiko upande wake. Hivyo, imeelekeza nguvu zake kutoka kwenye ubora wa kijeshi pekee kuelekea kwenye mfumo wa kutegemeyana kiuchumi duniani. Iran haina haja ya kuufunga Lango Bahari La Hormuz moja kwa moja; inatosha tu kuweka sharti kuwa usalama wa usafiri katika njia hiyo unategemea uwezo wake wa kutoa ushawishi na kuimarisha kanuni kwamba usalama wa Ghuba ya Uajemi hauwezi kuhakikishwa bila kuzingatia maslahi ya Tehran. Kwa mantiki hii, Lango Bahari La Hormuz linakuwa njia ya kidiplomasia ya kuilazimisha dunia kutambua nafasi ya Iran kikanda, badala ya kuwa tu chombo cha shinikizo la kijeshi.

Kwa utawala wa Kizayuni, hatari kubwa ipo katika ukweli kwamba kufanikiwa kwa mlinganyo huu kutaangamiza moja ya nguzo kuu za usalama wake: udhibiti wa kudumu wa Marekani juu ya mfumo wa usalama wa Mashariki ya Kati. Kwa miongo kadhaa, mkakati wa utawala huo dhalimu umejengwa juu ya dhana kwamba Marekani ina uwezo wa kulinda njia za biashara na nishati, kudhibiti nguvu za kikanda, na kusimamia kanuni za makabiliano. Ikiwa Iran itapata uwezo wa kuvuruga usafiri au kuainisha masharti ya meli kupita, itamaanisha kuwa uongozi wa kimkakati umehamia Tehran kutoka Washington.

Athari hizi hazishishii tu kwenye uga wa kijeshi; zinagusa pia mazingira ya kisiasa anayofanyia kazi adui Mzayuni. Kadiri gharama ya kukabiliana na Iran inavyoongezeka kwa uchumi wa dunia, ndivyo shinikizo la kimataifa linavyozidi ili kuepuka vita vikubwa na kutafuta maridhiano yanayozingatia maslahi ya Iran. Hali hii inaufanya utawala wa Kizayuni kukosa nafasi ya ujanja, kwani operesheni yoyote kubwa ya kijeshi itahukumiwa si kwa matokeo ya uwanja wa vita pekee, bali kwa athari zake kwenye usalama wa nishati na biashara ya kimataifa.

Kinyume chake, mzozo wa Lango la Hormuz unaipa Iran fursa ya kuimarisha nafasi yake miongoni mwa mataifa ya Ghuba ya Uajemi. Nchi hizi, licha ya kuendelea kuitegemea Marekani kiusalama, zinafahamu fika kuwa makabiliano yoyote ya wazi yataweka vituo vyao vya mafuta na bandari zao katikati ya moto. Ufahamu huu unapoongezeka, unazidisha haja kwa nchi za Ghuba ya Uajemi kufungua njia za maelewano na Tehran. Kwa mtazamo wa Tel Aviv, kudhoofika kwa muungano wa kikanda dhidi ya Iran ni pigo la kimkakati linalopunguza ufanisi wa mtandao wa ushirikiano ambao Marekani na utawala wa Kizayuni wamekuwa wakiujenga kwa miaka ya hivi karibuni.

Aidha, vita vya Lango la Hormuz havishishii Ghuba ya Uajemi pekee; vinafika hadi Bahari Nyekundu na Mlango wa Bab al-Mandab, ambapo Iran, kupitia washirika wake wa Mhimili wa Mapambano, inaweza kupanua shinikizo lake dhidi ya biashara ya kimataifa. Hii inazidisha changamoto kwa utawala wa Kizayuni, ambao unazidi kutegemea njia za baharini kwa biashara na mahitaji yake. Kadiri vitisho vya majini vinavyoongezeka, ndivyo utawala wa Kizayuni unavyolazimika kutawanya nguvu zake za kijeshi kwenye nyanja nyingi, jambo linaloongeza gharama za ulinzi.

Jambo muhimu zaidi ni kwamba mzozo huu unaashiria mabadiliko ya kimsingi katika asili ya nguvu za kikanda. Badala ya kutafuta udhibiti wa ardhi, Iran sasa inatumia jiografia yake kutoa ushawishi wa kisiasa. Ikiwa itafanikiwa kuimarisha kanuni kuwa usalama wa majini unapatikana tu kwa ridhaa yake, itapata nguvu inayovuka uwezo wake wa kijeshi, na kuipa nafasi kubwa ya kuathiri maamuzi ya mataifa makubwa duniani na kikanda.

Hivyo basi, mapambano ya Lango la Hormuz si vita vya njia ya maji pekee, bali ni vita vya kuamua utambulisho wa mfumo wa usalama katika Asia Magharibi. Kufanikiwa kwa Marekani kudhoofisha kadi ya Iran kutamaanisha kulinda mazingira ya kimkakati anayoyategemea Mzayuni. Lakini kufanikiwa kwa Iran kuufanya Lango la Hormuz kuwa chombo cha ushawishi kutaongeza nguvu ya mradi wake wa kikanda na kutengeneza eneo lenye nguvu mseto, ambapo ubeberu wa Marekani utafifia hatua kwa hatua na nafasi yake kuchukuliwa na mizani mipya ya nguvu.

Kwa mtazamo huu, Lango la Hormuz kwa utawala wa Kizayuni ni zaidi ya suala la bei ya mafuta; ni kipimo cha hatima ya mizani ya nguvu ambayo usalama wake umejengwa juu yake kwa miongo mingi. Mlango huo si lengo lenyewe la mzozo, bali ni silaha inayoweza kuchora upya ramani ya nguvu katika eneo hili na kuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa usalama wa utawala wa Kizayuni na mustakabali wa kimkakati wa Asia Magharibi.

3498396

captcha