IQNA – Watu kadhaa wametekwa nyara kutoka katika msikiti mmoja ulioko Jimbo la Niger, eneo la kaskazini-kati mwa Nigeria, na kundi la magaidi, kwa mujibu wa taarifa za wakazi na polisi.
Hili ni tukio la hivi punde la utekaji nyara wa watu wengi katika eneo ambalo limeshuhudia vitendo vya kikatili vya magenge ya wahalifu.
Wakazi wa eneo hilo wamesema idadi kubwa ya watu imetekwa, ambapo baadhi wanakadiria kuwa ni kati ya watu 60 hadi 80. Operesheni ya kuwaokoa waliotekwa nyara inaendelea.
Msemaji wa polisi, Wasiu Abiodun, alithibitisha kuwa washambuliaji hao walivamia Msikiti wa Kpenya, ulioko katika wilaya ya Dekara, eneo la serikali ya mtaa wa Borgu, mchana siku ya Ijumaa, baada ya awali kushambulia vijiji vya Gidan-Zana na Kpenya.
Ingawa Abiodun hakutoa idadi kamili ya waliotekwa, alibainisha kuwa hakuna maisha yaliyopotea katika shambulio hilo na kwamba vikosi vya jeshi vimepelekwa eneo hilo. Hadi sasa, hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na tukio hilo la kinyama.
Mwenyekiti wa Baraza la Borgu, Abdullahi Mohammed Nasir, amesema kuwa angalau watu 60 wametekwa, huku idadi isiyojulikana ya watu wakijeruhiwa kwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka.
“Waumini walikuwa wakiswali walipotekwa,” alisema Nasir. “Hapo ndipo watu hao waovu walipozingira msikiti na kuwachukua kwa nguvu.”
3498754