IQNA – Kutokana na changamoto za hali ya hewa nchini Singapore, vipindi vya hotuba za Swala ya Ijumaa vitafupishwa kwa muda kuanzia wiki hii.
Tangazo hilo limetolewa na Baraza la Kidini la Kiislamu la Singapore (MUIS).
“Kadiri hali ya hewa inavyozidi kuwa ya joto na baadhi ya maeneo ya Singapore yakianza kukumbwa na ukungu wa moshi, tunafanya marekebisho madogo lakini ya lazima katika hotuba zetu za Ijumaa,” lilieleza baraza la MUIS katika chapisho lake la Instagram siku ya Ijumaa (Agosti 21).
Kwa kawaida, hotuba ya kwanza huwa na urefu wa kurasa sita hadi saba, lakini kwa mabadiliko haya ya muda, hotuba hiyo itakuwa na chini ya kurasa nne, liliongeza baraza hilo.
“Tunatarajia kuwa hatua hii itasaidia kurahisisha kwa kiasi fulani mikusanyiko ya waumini, ibada, na kuwapa ahueni zaidi katika kipindi hiki cha changamoto za hali ya hewa.”
Vipindi hivyo vilivyofupishwa vitaendelea hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa.
Mapema wiki hii, Idara ya Hali ya Hewa ya Singapore ilibainisha kuwa mvua itakayonyesha katika nusu ya pili ya mwezi Agosti inatarajiwa kuwa chini ya wastani katika sehemu nyingi za Singapore.
Viwango vya juu vya joto kwa siku vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 33 na 34 katika siku nyingi, na kufikia hadi nyuzi joto 35 katika siku chache.
Singapore pia inaweza kukumbwa na hali ya ukungu wa moshi ikiwa moto wa misitu nchini Indonesia, hasa katika maeneo ya Sumatra na Kalimantan, utaongezeka.
Moshi unaotokana na moto huo wa kikanda unaweza kuathiri Singapore kutokana na upepo unaotarajiwa kuvuma kutokea kusini-mashariki au kusini-magharibi, iliongeza taarifa hiyo.
Idara ya Hali ya Hewa ilisema kuwa Wakala wa Mazingira wa Kitaifa utaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu na kutoa taarifa za mara kwa mara iwapo mazingira yatabadilika.
Kufikia saa 7 mchana siku ya Ijumaa, Kiashiria cha Viwango vya Uchafuzi (PSI) cha saa 24 nchini Singapore , ambacho ni kipimo cha ubora wa hewa , kilikuwa kati ya 60 na 74, hali inayowekwa katika kundi la “wastani.”
Ubora wa hewa huchukuliwa kuwa usiofaa kwa afya (unhealthy) wakati PSI inapozidi 100, hatari kwa afya (very unhealthy) ikizidi 200, na hatari kubwa (hazardous) inapozidi 300.
/3498731