Katika taarifa Jumatatu hii, Sadeq Hussein Jaber Ansari Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, mashambulio hayo mawili ya kigaidi, moja katika bustani mjini Lahore na nyingine katika uwanja wa michezo mjini Baghdad ni dalili ya wazi kuwa magaidi na wenye misimamo ya kufurutu ada hawawajali wala kuwaonea huruma raia wa kawaida wasio na hatua na kwamba hakuna eneo lolote linalosalimika na uovu wao.
Jaberi Ansari amesema kukaririwa hujuma za kigaidi maeneo mbali mbali duniani ni nukta inayokumbusha kuhusu udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka kimataifa ili kukabiliana na tatizo sugu la ugaidi na misimamo mikali.
Ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa magaidi wakufurishaji wa kundi la ISIS au Daesh walishambulia kwa bomu mechi ya soka katika uwanja mmoja mjini Iskanderiyah kusini mwa Baghdad na kupelekea watu wasiopungua 41 kupoteza maisha.
Aidha siku ya Jumapili watu 76 waliuawa na wengine zaidi ya 320 kujeruhiwa kwenye mripuko katika mji wa Lahore, kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kundi la kigaidi la Taliban limedai kuhusika na hujuma hiyo iliyopelekea idadi kubwa ya watoto na wanawake kuuawa katika Bustani ya Gulshan Iqbal katika mji huo muhimu nchini Pakistan.