Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam nchini Tanzania (JUWAKITA), Shamim Khan ambaye amehutubia sherehe hiyo amesema kuwa vazi la mwanamke wa Kiislamu la hijabu ni kito chenye thamani kubwa kwa wanawake na ngao inayowalinda wanawake Waislamu.
Shamim Khan amefafaanua kuhusu falsafa ya Hijabu katika Uislamu na kusema, hijabu haiishi katika vazi tu bali ni mtindo wa maisha na kielelezo cha utakasifu na heshima ya wanawake. Ameongeza kuwa wakati mwanamke anapolinda na kuheshimu vazi lake la Hijabu huweza kujiweka mbali matatizo mengi.
Mwenyekiti JUWAKITA amesema kuwa, utamaduni wa Magharibi hauwezi kumuokoa mwanamke wa Kiislamu bali unamharibu sambamba na kuangamiza na kueneza utovu wa haya na heshima katika jamii.
Sherehe hiyo ya Siku ya Hijabu ya Waridi nchini Tanzania imefanyika kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam Tanzania (JUWAKITA), ofisi ya Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Dar es Salaam na taasisi nyingine za Tanzania. Sherehe hiyo hufanyika kila mwaka kwa Munasaba wa Siku ya Hijabu Duniani ili kuhimiza umuhimu wa vazi la hijabu la mwanamke wa Kiislamu. Kila mwaka Februari mosi huadhimishwa kama Siku Hijabu Duniani.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘Siku ya Hijabu Duniani’ (World Hijab Day-WHD-), siku hii ilianzishwa na mkaazi wa New York Marekani, Bi. Nazma Khan kwa lengo la kuwahimiza watu kuwasilisha fikra za namna wafuasi wa dini mbali mbali wanavyoweza kuishi pamoja kwa maelewano na huo ndio msingi wa kuwaalika wasiokuwa Waislamu kuvaa Hijabu walau kwa siku moja.