IQNA

18:52 - January 21, 2020
News ID: 3472393
TEHRAN (IQNA) - Hatimaye wawakilishi wawili watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano makubwa ya Qur an tukufu ya Hifdh na Tajweed yatakayofanyika nchini Gabon, wamepatikana.

Kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la An Nuur la Tanzania, mmoja wa wawakilishi hao ni binti mdogo kabisa Ashura Aman Lilanga (19) aliyeibuka mshindi katika kundi la Hifdh huku kwa upande Tajweed, kijana Hosein Kesy, ndie aliyeibuka mshindi. 

Washindi hao kwa pamoja wamepata nafasi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania, katika mashindano ya kimataifa ambayo yatafanyika nchini Gabon, mwaka huu katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Kilele cha mchujo wa mashindano hayo ya kuwapata wawakilishi hao kilifanyika Jumamosi ya Januari 5, 2020, katika ukumbi wa Hotel ya Lamada, Ilala Jijini Dar es salaam, huku mgeni rasmi akiwa Mufti Sheikh Abubakari Zueir Bin Ally.

Mashindano hayo yameandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco, ambapo kwa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir ndio Rais wa Taasisi hiyo.

Akitoa nasaha zake kwa wawakilishi hao Mufti Zubeir, amewataka wawe watulivu pindi watakapoingia katika mashindano hayo na wala wasijitie wasiwasi na wasiwe na papara.

Mufti Zubeir aliwataka kuwa makini na wafanye juhudi katika kuhakikisha wanarudi na ushindi ambao ndio matarajio yao kwa ujumla na kuhakikisha bendera ya Tanzania inapeperuka kimataifa katika mambo ya kheri.

“Muwe watulivu pindi mtakapoingia katika mashindano msijitie wasiwasi, msiwe na papara muwe makini na mtoe juhudi zenu kuhakikisha kwamba mnapata ushindi na hayo ndio matarajio yetu mrejee nchini hali ya kuwa bendera ya Tanzania ipo juu.” Amesema Mufti Zubeir.

Mufti Zubeir, alisema mashindano hayo ni moja ya mashindano makubwa Afrika, hivyo ushiriki wa vijana hao kutoka nchini pamoja na juhudi zao katika kuihifadhi Qur an lakini pia kuna faida kubwa itakayopatikana kupitia wao nayo ni kuitangaza nchi yao kama Waislamu wa Tanzania, kimataifa kupitia Qur an Tukufu.

Alisema, miaka ya nyuma hapakuwa na wigo mpana wa kushiriki mashindano ya kuhifadhi Qur an Kimataifa na kuiwakilisha nchi, lakini kwa sasa inawezekana na matarajio ni kuitambulisha Tanzania Kimataifa kupitia usomaji wa Qur an.

Akawataka wawakilishi hao kutumia muda huu kujiandaa zaidi ili waweze kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo kwani macho na masikio ya Waislamu Tanzania siku hiyo yataelekezwa nchi Gabon, huku wakiwaombea dua.

Mufti Zubeir, alisema katika mashindano ya mwaka huu nchini Gabon, Tanzania imebahatika kutoa Jaji mmoja atakaeshiriki katika jopo la Majaji katika mashindano hayo, akasema hilo pia ni jambo kubwa kwani katika mashindano yaliyopita Tanzania, haiku pata nafasi hiyo.

Awali Katibu wa Taasisi hiyo ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco, tawi la Tanzania, Sheikh Mussa Hemed, akiongea katika hafla hiyo, alisema mwaka jana mashindano hayo yalifanyika nchini Morocco, ambapo nchi 36 za Bara la Afrika zilishiriki na Tanzania iliwakilishwa na vijana wawili.

Alisema, mashindano wanayokwenda kushiriki vijana hao ni mashindanoi makubwa na yenye kuzingatia vigezo vya hali ya juu katika Hifdh na Tajweed.

An Nuur

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: