IQNA

Hofu ya Corona: Sala ya Ijumaa yasitishwa katika Msikiti wa Paris

16:10 - March 10, 2020
Habari ID: 3472551
TEHRAN (IQNA) – Msikiti wa Jamia wa Paris, Ufaransa umetangaza kusitishwa kwa muda sala ya Ijumaa katika msikiti huo kutokana na hofu ya kuenea ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama Corona.

Katika taarifa, mkuu wa bodi ya wasimamizi wa msikiti huo Shamseddin Hafiz amesema: "Uamuzi huu umechukuliwa kama tahadhari ya kuzuia kuenea kirusi kipya cha corona."

Hatahivyo amesema sala za jamaa zitaendelea msikitini humo kama kawaida. Msikiti wa Jamia wa Paris ( Grande Mosquée de Paris ) uko katika Wilaya ya 5 na ni kati ya misikiti mikubwa zaidi Ufaransa. 

Wiki iliyopita, hotuba za sala ya Ijumaa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hazikupindukia dakika 10 kufuatia amri ya Idara ya Masuala ya Kiislamu na Wakfu nchini humo. Amri hiyo imetolewa ikiwa ni katika hatua zilizochukulia kama tahadhari kuzuia kuenea kirusi cha COVID-19.

 Saudi Arabia nayo imewapiga marufuku raia wake na wakazi wa nchi hiyo kutekeleza ibada ya Umrah katika mji Mtakatifu wa Makka au kuzuru Msikiti wa Mtume SAW katika mji wa Madina kwa hofu ya kuenea kirusi cha Corona ambacho kinaenea kwa kasi duniani.

Maambukizo ya corona yameshaziathiri sasa nchi 115 ikiwemo China. Aidha zaidi ya watu 115,000 duniani wameambukizwa virusi hivyo; ambapo miongoni mwao zaidi ya watu elfu 64 wamepona na zaidi ya elfu nne wengine wamepoteza maisha.

3470878

captcha