IQNA

15:11 - April 24, 2020
Habari ID: 3472698
TEHRAN (IQNA)- Hivi karibuni klipu ya video ya qiraa ya Qur’ani Tukufu ya Ustadh Abdul Basit Abdul Samad imesambaa katika intaneti.

Katika klipu hii ambayo ilirekodiwa mwaka 1985 katika Msikiti wa Khalid bin Walid mjini Cairo, Misri, anasoma  Surah al-Fath na aya za 1-9 za Surah al-Hujurat  katika Qur’ani Tukufu.

Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikuwa miongoni mwa maqarii na wasomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu na weledi wa masuala ya Qur'ani wanamtambua kuwa ndiye qarii mkubwa zaidi wa Qur'ami kote duniani. Ustadh Abdus Samad alibuni na kuanzisha mbinu makhsusi ya kiraa ya Qur'ani.

Abdul Basit alizaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Almazaizah katika eneo la Armant kusini mwa Misri. Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikamilisha hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10 kijijini kwake kwa Ustadh Al Amir na akahitimu aina zote za kiraa ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 14.

Abdul Basit alipewa lakabu ya 'Koo ya Dhahabu' kutokana na kiraa yake ya kuvutia na alipendwa mno na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kwa kadiri kwamba hadi sasa anatambuliwa kuwa qarii mashuhuri na anayepesndwa zaidi wa Qur'ani.

Qiraa ya Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Aidha inadokezwa kuwa nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.

Mwishoni mwa umri wake, Sheikh Abdul Basit alipatwa na maradhi ya kisukari na baadaye uvimbe wa ini. Alipelekwa London Uingereza kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa na maradhi na kurejeshwa Cairo wiki mbili baadaye. Inasemekana kwamba Sheikh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa amehisi kwamba siku zake za kuishi duniani zinakaribia ukingoni na wakati wa kukutana na Mola Muumba ulikuwa unakaribia.

Qari huyo mashuhuri wa Misri aliaga dunia tarehe 30 Novemba mwaka 1988 katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Sheikh Abdul Basit ameacha kanda nyingi za Sauti ya qiraa yake ya Qur'ani Tukufu ambazo bado zinawavutia wengi wengi duniani.

3892755

 

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: