IQNA

Rais wa Iran katika mazungumzo ya simu na rais wa Afrika Kusini

Ulazima wa ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na vikwazo vya Marekani

22:26 - April 28, 2020
Habari ID: 3472711
TEHRAN (IQNA)- Marais wa Iran na Afrika Kusini wamesisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja za biashara na uchumi na pia wakasema kuna udharura wa kubadlishana uzoefu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona sambamba kuboresha ushirikiano wa kiafya na kisayansi.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wameyasema hayo Jumanne katika mazungumzo ya simu. Marais hao wawili wameashiria historia nzuri ya ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili na kusema kuna udharura wa kutafutwa uwezo mpya kwa ajili ya kupanuliwa uhusiano huu na kutekelezwa miradi ya pamoja.

Aidha marais wa Iran na Afrika Kusini wamesisitiza kuhusu kuimarishwa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na vikwazo vilivyo  dhidi ya binadamu vya Marekani. Pia wametilia mkazo suala la kukabiliana na jinai zinazokiuka ubinadamu ambazo zinatendwa dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina na hali kadhalika kuwepo jitihada za kurejesha amani na utulivu katika nchi za Syria na Yemen.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais Rouhani ameashiria hatua zilizo kinyume cha  ubinadamu za Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Pamoja na kuwepo janga la ugonjwa wa corona kote duniani, Marekani imeshadidisha vikwazo vyake vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran." Rais wa Iran amesema Marekani inakiuka sheria za kimataifa na kanuni  za afya duniani  ambapo inazuia hata bidhaa za kiafya na kitiba kufika Iran."

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uanachama usio wa kudumu wa Afrika Kusini katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: "Inatazamiwa kuwa, Afrika Kusini itapinga sera za maamuzi ya upande mmoja ya Marekani katika Umoja wa Mataifa na katika uga wa kimataifa kwa ujumla sambamba na kusisitiza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kinyume cha sheria."

Kwa upande wake, Rais wa Afrika Kusini amelaani hatua zinazokiuka uadilifu na sheria za Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Nchi zote za dunia zinapaswa kuchukua hatua dhidi ya adui wa  pamoja, yaani corona na hivyo hakupasi kuwepo vikwazo na mashinikizo ambayo yataibua matatizo katika mataifa mengine.

3895019

captcha