IQNA

Jeshi la Nigeria ladondosha mabomu katika ngome ya magaidi wa Boko Haram

15:17 - July 20, 2020
Habari ID: 3472982
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Nigeria limetangaza kuwaangamiza magaidi 8 wa ngazi za juu wa kundi la Boko Haram.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria John Enenchi amesema magaidi hao wameuawa katika hujuma iliyotekelezwa kwa ndege za kivita katika kijiji cha Goski jimboni Borno.

Kwingineko, magenge ya wabeba silaha wameua wanajeshi wasiopungua 23 nchini Nigeria katika kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa zinasema hujuma hiyo ya kuvizia ilijiri Jumapili usiku wakati wanajeshi hao walipokuwa wakipita katika eneo la msitu la Wilaya ya Jibia jimboni Katsina.

Duru za kijeshi zinasema miili 23 ya wanajeshi hao imepatikana huku baadhi ya wanajeshi wakiwa hawajulikani waliko. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo.

Magenge ya wabeba silaha ambayo yamekuwa yakijihusisha na wizi wa mifugo na utekaji nyara yameongezeka kaskazini mwa Nigeria na wataalamu wanaonya kuwa yamkini magenge hayo sasa yanashirikiana na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Siku ya Jumamosi pia katika eneo hilo hilo, watoto watano waliuawa na wengine sita kujeruhiwa wakati bomu lililoplipuka. Haijabainika ni nani aliyetega bomu hilo.

Jimbo la Katsina, anakotoka Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, linakabiliwa na tatizo kubwa la umasikini na limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya wahalifu na magaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Ni zaidi ya muongo mmoja sasa ambapo, eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya wanachama wa kundi la kigaidi Boko Haram.

Zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009. Magaidi hao wakufurishaji pia wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon.

3910987

Kishikizo: nigeria boko haram
captcha