IQNA

India yawakandamiza watu wa Kashmir katika kumbukumbu ya Agosti 5

20:30 - August 05, 2020
Habari ID: 3473038
TEHRAN (IQNA) - Serikali ya India imepiga marufuku watu kutoka nje katika eneo la Kashmir na kuweka hatua kandamizi za usalama wakati huu kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu New Delhi ilipofuta mamlaka ya utawala wa ndani katika eneo hilo lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu.

India ilianza kutekeleza sheria hizo kali Jumatatu baada ya taarifa za kipelelezi kuonesha kuwa, Waislamu wa Kashmir wanajiandaa kufanya maandamano na migomo ya kupinga hatua ya serikali ya India ya kufuta mamlaka ya ndani ya eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya India imesema sheria za marufuku ya kutoka nje zinatekelezwa tarehe 4 na 5 Agosti katika mji wa Srinagar.

Mwezi Agosti mwaka jana Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.

Uamuzi wa India wa kufuta mamlaka ya utawala wa ndani ya Kashmir umekanyaga haki ya kimsingi ya watu wa eneo hilo kiasi kwamba, umepingwa na kukemewa hata na wajumbe wa ngazi za juu wa chama tawala cha BJP.

Amri ya sasa ya serikali ya India dhidi ya watu wa Kashmir inafanana na ile iliyotekelezwa kabla ya kufutwa mamlaka ya utawala wa ndani ya Kashmir tarehe 5 Agosti mwaka jana. Wakati huo India ilikata mawasiliano yote ya simu na mtandao wa intaneti na kusambaza maelfu ya wanajeshi katika maeneo mbalimbali ya Kashimir.

Wakazi wa Kashimir wametoa wito wa kutambuliwa siku ya tarehe 5 Agosti kuwa ni siku nyeusi katika historia ya eneo hilo.  

Mgogoro wa Kashmir ulianza wakati Pakistan na India zilipotengana mwaka 1947 baada ya kuondoka mkoloni Muingereza ambaye alipanda mbegu za chuki baina ya mataifa hayo mawili. Wakazi wa eneo la Kashmir linalotawaliwa na India wanataka kura ya maoni iainishe hatima yao ya ama kubakia India, kupata uhuru kamili au kujiunga na Pakistan. India inapinga vikali pendekezo hilo la kura ya maoni ya kuamua hatima ya Kashmir, eneo ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu. 

3472198

captcha