IQNA

Ongezeko la kauli za chuki nchini India baada ya shambulio la Pahalgam

20:41 - May 04, 2025
Habari ID: 3480633
IQNA-Ripoti mpya ya Taasisiya India Hate Lab (IHL) imebaini ongezeko kubwa la matukio ya hotuba na kauli za chuki katika maeneo mbalimbali nchini India kufuatia shambulio la kigaidi lililotokea Pahalgam, Jammu na Kashmir, mnamo Aprili 21.

Shambulio hilo, ambalo liliwaua watalii 26, lilizua mshtuko mkubwa na kulaaniwa vikali. Hata hivyo, matukio ya hotuba za chuki yaliongezeka kuanzia Aprili 22 hadi Mei 2, huku jumla ya matukio 64 yakirekodiwa katika majimbo tisa na eneo la Jammu na Kashmir.

Maharashtra iliongoza kwa idadi kubwa ya matukio haya, ikifuatiwa na Uttar Pradesh, Uttarakhand, Haryana, Rajasthan, Madhya Pradesh, Himachal Pradesh, Bihar, na Chhattisgarh. Ripoti inaeleza kuwa makundi ya Wahindu au mabaniani wenye misimamo mikali kama Vishwa Hindu Parishad (VHP), Bajrang Dal, Antarrashtriya Hindu Parishad (AHP), na Rashtriya Bajrang Dal (RBD) yalihusika katika kuandaa mikusanyiko yenye maudhui ya uchochezi dhidi ya Waislamu.

Katika mikutano hiyo, viongozi wa kisiasa na wanaharakati walitumia lugha kali ya kuchochea ghasia na ubaguzi wa kijamii na kiuchumi. Ripoti inabainisha kuwa baadhi ya wanasiasa, akiwemo mbunge wa chama tawala  cha Bharatiya Janata (BJP), walihudhuria matukio hayo na kuunga mkono wito wa kuwazuia Waislamu kushiriki katika shughuli za kiuchumi, pamoja na kueneza nadharia za njama dhidi ya jamii hiyo.

IHL inatahadharisha kuwa vikundi hivi vinatumia tukio la Pahalgam kama sababu ya kuchochea mgawanyiko wa kijamii na kuendeleza harakati za uhasama. Ripoti inaonyesha jinsi matukio haya yanavyoathiri mshikamano wa kitaifa na kuhamasisha chuki inayoweza kusababisha vurugu zaidi.

3492926

captcha