IQNA

Hania amemtaka Biden aufutilie mbali mpango wa Marekani-Wazayuni wa Muamala wa Karne

14:40 - November 08, 2020
Habari ID: 3473341
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amemtaka rais mteula wa Marekani Joe Biden aufutilie mbali mpango wa Marekani-Wazayuni wa Muamala wa Karne, uliojaa njama na hila kwa madhara ya Wapalestina.

Aidha Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ametoa mwito kwa Rais mteule wa Marekani aiangalie upya kadhia ya kuhamishiwa ubalozi wa Marekani mjini Quds kutoka Tel Aviv, kinyume na sheria na maazimio ya kimataifa.

Halikadhalika ameashiria kuhusu kubwagwa Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa Marekani na kusema kuwa, rais wa Marekani aliyetaka kuisambaratisha kadhia ya Quds ametokomea, lakini Baitul Muqaddas itaendelea kuwepo daima.

Ismail Hania amebainisha kuwa, kuuunga mkono utawala wa Kizayuni ni katika sera madhubuti za Marekani, lakini amemtaka rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden kuhitimisha sera hizo za kidhalimu dhidi ya wananchi wa Palestina.

Mpango uliojaa njama uliobuniwa na Marekani na Wazayuni wa Israel uliopewa jina la Muamala wa Karne ulizinduliwa Januari 28 mwaka huu katika kikao kati ya Rais anayeondoka wa Marekani Donald Trump na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa mpango huo, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa tena na haki ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu aradhi zilizosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.

3933845

captcha