Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amenukuliwa akisema kwamba makubaliano yalitiwa saini kati ya Palestina na utawala wa Israel, ambayo yalisimamiwa na Washington.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mateka wote lazima waachiliwe katika hatua tatu na Hamas imetekeleza ahadi zake zote katika hatua ya kwanza, lakini utawala unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina unakwepa kuheshimu ahadi zake katika hatua ya pili.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya usitishaji vita serikali ya Marekani inabidi iushinikize utawala wa Kizayuni uanze awamu ya pili ya makubaliano hayo.
Msemaji huyo wa Hamas ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni huenda ukatumia vyema matamshi ya hivi karibuni ya Trump ya kuendeleza mzingiro wa Gaza na siasa za kuwatesa kwa njaa wakazi wa Gaza kwa kasi kubwa zaidi.
Ameeleza kuwa, njia bora zaidi ya kuwaachilia huru mateka waliosalia wa Israel ni utawala wa Kizayuni kuingia katika awamu ya pili ya mazungumzo na kuulazimisha utawala huo uheshimu makubaliano yaliyopo.
Leo Alkhamisi asubuhi, rais wa Marekani ametishia kwamba kama Hamas hawatafanya anachosema, hakuna mwanachama yoyote wa Muqawama atabakia salama. Vitisho kama hivyo aliwahi kuvitoa huko nyuma rais huyo mpenda migogoro wa Marekani.
Njama za Israel za kudhibiti misaada inayoingia Gaza
Maafisa kutoka mashirika matano makubwa ya misaada duniani na Umoja wa Mataifa wameonya leo Alkhamisi asubuhi kuhusu njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuchukua udhibiti wa moja kwa moja wa misaada ya kibinadamu inayoingia kwenye Ukanda wa Gaza.
Gazeti la Washington Post limewanukuu maafisa hao wa mashirika matano tofauti ya misaada ya kibinadamu duniani na kuandika: "Israel inafanya njama za kudhibiti moja kwa moja misaada inayoingia huko Gaza na suala zima la usambazaji wa misaada hiyo."
Ripoti hiyo inasema: "Chini ya mpango wa Israel, ni sehemu moja tu ya kivuko cha Karm Abu Salem, ndiyo itakayoachwa wazi kwa ajili ya kuingia misaada ya kibinadamu huko Gaza na kwamba mfumo wa kufuatilia misaada hiyo utaanzishwa na viongozi wa Israel kwa ajili ya kudhibiti usambazaji wa misaada ndani ya Ghaza."
Hayo yamekuja huku Hamas ikisema kwamba imepokea vizuri mpango wa nchi za Kiarabu wa kuikarabati na kuijenga upya Gaza. Mpango huo ni ule uliopitishwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri. Mpango huo pia unakusudia kuzuia kuondolewa Wapalestina katika eneo hilo lililoko chini ya mzingiro mkali na wa kila upande wa Wazayuni.
Hamas imesema katika taarifa yake kwamba, mkutano wa Cairo umeashiria hatua muhimu kuelekea kupatikana sauti moja ya Waarabu na Waislamu kwa kadhia ya Palestina, hasa wakati huu ambapo Israel inaendelea kushambulia na kuwahamisha watu kwenye makazi yao huko Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds.
Hamas yaunga mkono msimamo wa nchi za Kiarabu
Wakati huo huo Hamas imekaribisha mpango wa kuikarabati na kuijenga upya Gaza, uliopitishwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri. Mpango huo pia unakusudia kuzuia kuondolewa Wapalestinakatika eneo hilo lililo chini ya mzingiro.
Hamas imesema katika taarifa yake kwamba, mkutano wa Cairo unaashiria hatua muhimu kuelekea kupatikana sauti moja ya Waarabu na Waislamu kwa kadhia ya Palestina, hasa wakati huu ambapo Israel inaendelea kushambulia na kuwahamisha watu kwenye makazi yao huko Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds.
Kundi hilo la Muqawama limewapongeza viongozi wa Kiarabu kwa kutoafiki majaribio ya kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao, au kudhoofisha kadhia yao ya kitaifa, na kuiita taarifa ya Cairo 'ujumbe wa kihistoria' kwamba Nakba ya pili (Janga), haitaruhusiwa.
Hamas imekaribisha wito wa kususiwa Israel kibiashara na kisiasa, ikisisitiza kuwa hiyo ndiyo "hatua ya kimkakati yenye ufanisi ya kuitenga Israel na kuishinikiza kufuata sheria za kimataifa."
Jumanne, Machi 4, mji mkuu wa Misri, Cairo, ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliolenga kujadili matukio ya hivi karibuni kuhusu suala la Palestina na kufikia uamuzi wa pamoja wa Kiarabu kuhusu Ukanda Gaza.
Viongozi wa Kiarabu walioshiriki katika mkutano huo, hususan Misri na Jordan, walisisitiza uungaji mkono wao kwa mpango wa ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza na kupinga kurejea kwa vita na uhamishaji wa Wapalestina kwa nguvu.
Katika mkutano huo, viongozi wa Kiarabu walipitisha mpango wa dola bilioni 53 kwa ajili ya ujenzi upya wa Gaza. Mpango huu ni kinyume na mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa "kuchukua usimamizi wa Gaza" na kuwahamisha kwa nguvu zaidi ya Wapalestina milioni mbili.
4270062