IQNA

Ansarullah ya Yemen yataka Waislamu wauhami Msikiti wa Al Aqsa

16:29 - December 23, 2020
Habari ID: 3473483
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Wananchi wa Yemen ameashiria kuendelea kuchimbwa mashimo na njia za chini kwa chini kuelekea katika msikiti mtakatifu wa al-Aqswa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kueleza kwamba, Waislamu wanapaswa kutumia nyenzo na suhula zote kukabiliana na njama hizo.

Muhammad Ali al-Houthi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba, kuna haja kwa Waislamu kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kukabiliana na hatua haribifu za Wazayuni pamoja na uchimbaji wa mashimo na njia za chini kwa chini kuelekea katika msikiti huo.

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Wananchi wa Yemen  ameutaka Umma wa Kiislamu kutohadaika na propaganda za maadui, mamluki na vibaraka wao zenye lengo za kuzipotosha fikra za Waislamu na kadhia yao ya kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu ambayo ni Palestina.

Amesema, msikiti wa al-Aqswa uko hatarini hivyo kuna haja kwa Waislamu kutumia nyenzo na suhula zote walizonazo kwa ajili ya kuuhami na kuulinda.

Itakumbukwa kuwa, tangu utawala dhalimu wa Israel ulipouvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji mtakatifu wa Quds mwaka 1967 hadi sasa, umekuwa ukichimba mashimo ya chini ya ardhi katika mji huo hasa katika eneo lake la kale na kandokando mwa Msikiti wa Al-Aqswa ili kuwalazimisha Wapalestina wayahame maeneo hayo na kuweza kuyadhibiti maeneo yanayozunguka msikiti huo mtakatifu.

Lengo la utawala vamizi wa Israel la kuchimba mashimo ya njia za chini ya ardhi chini ya Msikiti wa Al-Aqswa ni kufuta nembo na athari za Kiislamu na za kihistoria za taifa la Palestina.

3473492

captcha