IQNA

Ripoti

Ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

13:53 - September 15, 2021
Habari ID: 3474298
TEHRAN (IQNA)- Kuenea chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika nchi za Magharibi hivi sasa limegeuka na kuwa tatizo kubwa na la kijamii, tatizo ambalo limeibua na kushadidisha vitendo vya utumiaji mabavu katika jamii ya Magharibi.

Vitendo vichafu vya kampeni za chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni huko nchini Marekani na barani Ulaya. Katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa Ulaya walifanya kila wawezalo kuwafungamanisha na ugaidi Waislamu wanaoishi barani humom na hivyo kuhalalisha mapungufu ya kiusalama na kisiasa yanayoisumbua jamii ya Magharibi. Katika uga huu tunaweza  kuashiria matukio kama ya kuvunjiwa heshima Mtume (saw), Qur’ani Tukufu, kuwapachika jina la ugaidi Waislamu, kuamiliana vibaya na wafuasi wa dini ya Uislamu, utumiajui mabavu na ubaguzi wa polisi dhidi ya Waislamu na kupasishwa sheria  ambazo kimsingi zinalenga kuwabana na kuwakandamiza Waislamu.

Mashinikizo haya yamewafanya hata baadhi ya viongozi wa Ulaya wajitokeza na kuelezea wasiwasi walionao kuhusiana na mashinikizo dhidi ya Waislamu na kulitaja hilo kama chimbuko la kukua harakati za wafuasi wa mrengo wa kulia na wenye misimamo ya kuchupa mipaka, na vilevile kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu katika mataifa hayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya kundi la Waislamu katika Bunge la Uingereza ni kuwa, kuenea chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya kumepelekea kushadidi tofauti za kimatabaka katika jamii na kukithiri uhalifu unaohusiana na chuki na mashambulio ya kigaidi. Sehemu moja ya ripoti hiyo inabainisha kwamba: Fikra za waliowengi nchini Uingereza zimekuwa na mtazamo wa kiubaguzi kuhusiana na itikadi za Waislamu na hilo limetokana na utoaji hukumu wa kabla hata ya kufanya kosa unaofanywa dhidi ya wafuasi wa dini hii tukufu.

Gazeti la The Guardian la Uingereza hivi karibuni lilitahadharisha kwamba, chuki dhidi ya Uislamu (Isamophobia) zimeongezeka nchini Uingereza na kumekuwa kukifanyika mibinyo ya kuratibiwa dhidi ya Waislamu.

Hali hii imevifanya vyama vya mrengo wa kushoto na wanasiasa wa polisi katika nchi za Ulaya  kama Ujerumani na Ufaransa kutumia vibaya hali hii na kwa kuzingatia kukaribia chaguzi katika mataifa hayo, wanalitumia hilo kama karata ya kupata kura na hivyo kufungua vinywa vyao na kuwataja Waislamu kama chanzo cha ugaidi, tatizo la ajira na ukosefu wa usalama na amani katika nchi hizo.

Katika uwanja huo, nchini Ufaransa Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo akiwa na lengo la kuwaridhisha wapiga kura wamchague katika uchaguzi ujao miezi michache ijayo sambamba na kutumia msamiati wa "Ugaidi wa Kiislamu" ametangaza kuunga mkono kikamilifu sheria zinazowabana Waislamu. Nchini Ujerumani pia hivi karibuni kulipasishwa sheria ambayo inapiga marufuku mabinti wa Kiislamu kuvaa vazi tukufu la hijabu wakiwa katika idara za serikali na vituo vya polisi.

Nchini Canada na Marekani pia kumeshuhidiwa ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu hasa katika mwezi huu wa kumbukumbu ya matukio ya Septemba 11.

Hii ni katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni kutokana na masaibu ya janga la Covid-19, mabadiliko ya kisiasa na kushadidi matatizo ya kiuchumi ulimwenguni kote, vitendo vya utumiaji mabavu katika jamii ya Magharibi vimeshadidi mno. Picha zilizosambazwa hivi karibuni nchini Ufaransa zikionyesha wananchi wakiandamana kulalamikia sheria kali za kukabiliana na janga la Corona ni mfano wa wazi kuhusiana na jambo hili.

Filihali Ulaya na ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla yanakabiliwa na tatizo kubwa katika uga wa usalama na siasa. Malalamiko ya kijamii yameongezeka mno katika mataifa hayo na bila shaka madai yao ya uhuru wa kutoa maoni, utendaji wa chuki dhidi ya Uislamu na kanuni kali za kuwabinya Waislamu wanaoishi katika nchi hizo ni mambo ambayo hayakubaliwi tena na fikra za waliowengi katika nchi hizo. Hiyo ni hatari ambayo sasa baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Ulaya wameidiriki na kutoa indhari kuhusiana nayo.

3996627/ 3996669

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha