IQNA

Hamas yalaani kukamatwa Khatibu wa Msikiti wa Al Aqsa

16:07 - October 11, 2021
Habari ID: 3474409
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amelaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nyumba ya Sheikh Ikrima Sabri na kusisitiza kuhusu mshikamano wa Wapalestina katika kutetea Mji wa Quds (Jerusalem) na Msikiti wa Al Aqsa ulio mjini humo.

Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Khatibu wa Msikiti wa Al Aqsa Sheikh Ikrima Sabri. Haniya amesema hujuma ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nyumba ya mwanazuoni huyo wa Kiislamu na kumsaili kwa masaa sita ni muendelezo wa ukandamizaji wanazuoni wa Kiislamu na shakhsia wa kidini Wapalestina katika mji wa Quds. Aidha amemtaja Sheikh Sabri kuwa mmoja kati ya watetezi wakubwa zaidi wa Msikiti wa Al Aqsa.

Haniya ametangaza kufungamana na Maulamaa Wapalestina na wakaazi wa mji wa Quds na kuongeza kuwa, kwa kuzingatia kuwa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni yana uhusiano wa karibu, ni wazi kuwa misimamo yao hasimu dhidi ya Palestina haitabadilika.

Haniya pia amesema Hamas imewataka wapatanishi Wamisri wamshinikize adui Mazayuni asitishe hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa huku akitoa tahadhari kuhusu kuendelea hujuma za Wazayuni maghasibu.

Siku ya Jumapili, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliishambulia nyumba ya Sheikh Ikrima Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al Aqsa na kumsaili kwa masaa sita. Hadi sasa Sheikh Sabri amekamatwa mara kadhaa na askari wa utawala wa Kizayuni kwa visingizo mbali mbali kama vile kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina, kupinga wazi wazi uanzishwaji uhusiano wa kawaida baina ya baadhi ya nchi na utawala wa Kizayuni na pia kutokana na upinzani wake kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. 

4003863

captcha