IQNA

Kadhia ya Palestina

Maelfu ya Wapalestina wakaidi Vizuizi vya Israeli, waswali Tarawehe katika Msikiti wa Al-Aqsa

16:08 - March 23, 2024
Habari ID: 3478560
IQNA - Wakati utawala haramu wa Israel umeweka vikwazo vya kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa katika mji mtakatifu wa al-Quds, zaidi ya waumini 100,000 wa Kipalestina walishiriki katika Swala maalum ya mwezi wa Ramadhani kwenye msikiti huo siku ya Ijumaa.

Wapalestina walishiriki katika sala ya usiku ya Tarawehe, ambayo ni ibada maalumu ya Waislamu wa madhehebu ya Ahul Sunna ambayo huswaliwa usiku katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Idara ya Wakfu za Kiislamu mjini al-Quds (Jerusalem) imesema zaidi ya waumini 100,000 walihudhuria sala hiyo katika Ijumaa ya pili ya Ramadhani.

Shirika rasmi la habari la Palestina, WAFA, lilisema kuwa vikosi katili vya Israel viliwekwa kwa wingi katika Mji Mkongwe wa Al Quds katika jaribio la kuzuia waumini kufika katika msikiti huo.

Imeongeza kuwa mamlaka ya Israel inaendelea kupiga marufuku timu za Hilali Nyekundu ya Palestina kujenga kliniki yake katika msikiti huo ili kutoa huduma za matibabu kwa waumini.

Tel Aviv imewawekea vikwazo waumini wa Kipalestina kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya jeshi la utawala wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyoanza Oktoba 7.

Mashambulio hayo ya Israel yameua zaidi ya Wapalestina 32,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Msikiti wa Al-Aqsa ni eneo la tatu kwa utakatifu duniani kwa Waislamu. Wayahudi huliita eneo hilo kuwa eti ni Mlima wa Hekalu, wakidai kuwa palikuwa na mahekalu mawili ya Kiyahudi katika nyakati za kale.

Israel iliikalia kwa mabavu al-Quds Mashariki, ambako unapatikana Msikiti wa Al-Aqsa, wakati wa Vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1967. Ilitwaa jiji lote mwaka wa 1980 katika hatua ambayo haijatambuliwa kamwe na jumuiya ya kimataifa.

3487694

Habari zinazohusiana
captcha