IQNA

Magaidi wa Daesh washambulia msikiti jijini Islamabad na kuua angalau watu 31

8:06 - February 07, 2026
Habari ID: 3481895
IQNA- Mlipuko mkubwa umetikisa msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika viunga vya mji mkuu wa Pakistan wakati wa sala ya Ijumaa, na ambapo watu wasiopungua 31 wameuawa shahidi huku wengine wasiopungua 169 wakijeruhiwa. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limetangaza kuhusika na hujuma hiyo.

Kulikuwa na hofu kwamba idadi ya waliopoteza maisha kutokana na mlipuko katika msikiti wa Khadija al-Kubra mjini Islamabad huenda ikaongezeka, kwani baadhi ya majeruhi waliripotiwa kuwa katika hali mahututi. Picha za televisheni na mitandao ya kijamii zilionyesha polisi na wakazi wakibeba majeruhi kuwapeleka katika hospitali za karibu.

Waokoaji pamoja na majeruhi walielezea tukio hilo kuwa la kutisha na lenye vurugu nyingi, huku miili ya waumini ikionekana ikiwa imetapakaa juu ya sakafu ya msikiti iliyofunikwa mazulia.

Hussain Shah alisema alikuwa akiswali katika uwanja wa nje wa msikiti pale mlipuko mkubwa na wa ghafla ulipotokea. “Mara moja nilihisi kuwa shambulio kubwa sana limetokea,” aliambia shirika la habari la AP.

Alipoingia ndani ya msikiti, Shah alisema alikuta majeruhi wengi wakipiga mayowe na kuomba msaada. Alisema alihesabu takriban miili 30 ndani ya msikiti, huku idadi ya waliojeruhiwa ikionekana kuwa kubwa zaidi.

Mtu mwingine aliyesikika katika kipande cha video kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii alisema kulikuwa na washambuliaji wasiopungua wawili, ambao walifyatua risasi kwa waumini kabla ya kujilipua kwa mabomu. “Watu walikuwa wamelala kwenye madimbwi ya damu. Niliona vichwa na viungo vya miili vikitenganishwa na miili yao,” alisema.

Kundi la kigaidi la ISIS, linalojulikana pia kama Daesh, lilidai kuhusika na shambulio hilo kupitia kituo chake cha Telegram. Kundi hilo limehusishwa na mashambulio ya awali dhidi ya waumini wa Kishia nchini Pakistan.

Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, na Waziri Mkuu, Shehbaz Sharif, wamelaani shambulio hilo katika taarifa tofauti na kutoa rambirambi zao kwa familia za marehemu. Viongozi hao waliagiza kuwa msaada wote wa kitabibu utolewe kwa majeruhi bila kuchelewa.

“Kuwalenga raia wasio na hatia ni jinai dhidi ya ubinadamu,” alisema Zardari. “Taifa linasimama pamoja na familia zilizoathiriwa katika kipindi hiki kigumu.”

Sharif alisema ameamuru uchunguzi wa kina ufanyike. “Waliohusika lazima watambuliwe na waadhibiwe ipasavyo,” alisema.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, naye pia alilaani shambulio hilo na kuagiza mamlaka husika kuhakikisha majeruhi wanapatiwa huduma bora zaidi za matibabu.

Habari inayohusiana:

Shambulio la Ijumaa lilitokea wakati Rais wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev, aliyekuwa katika ziara rasmi ya siku mbili nchini Pakistan, akihudhuria hafla moja mjini Islamabad pamoja na Sharif. Hafla hiyo ilikuwa umbali wa maili kadhaa kutoka eneo la msikiti.

Mojawapo ya mashambulio mabaya zaidi kuwahi kutokea Islamabad lilitokea mwaka 2008, pale gaidi alipolenga hoteli ya Marriott, na kuua watu 63 huku zaidi ya 250 wakijeruhiwa. Mnamo Novemba mwaka jana, gaidi mwingine alijilipua nje ya jengo la mahakama mjini Islamabad, na kuua watu 12.

Shambulio la hivi karibuni linajiri takribani wiki moja baada ya kundi lililopigwa marufuku la Balochistan Liberation Army kutekeleza mashambulio katika jimbo la Balochistan kusini-magharibi mwa nchi, na kuua takribani watu 50. Kwa mujibu wa jeshi la Pakistan, vikosi vya usalama vilijibu kwa kuwaua zaidi ya “magaidi” 200.

3496317

captcha