IQNA

Al-Azhar yatoa wito kwa viongozi wa dunia kusitisha mapigano Ukraine

11:31 - February 27, 2022
Habari ID: 3474984
TEHRAN (IQNA) –Sheikhe mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al-Ahzar nchini Misri ametoa wito kwa Russia na Ukraine kusikiliza wito wa kumaliza vita kati ya nchi hizo mbili.

Katika taarifa iliyotolewa kwa Kiarabu na Kiingereza, Sheikh Ahmed El-Tayyeb pia alitoa wito kwa viongozi wa dunia na taasisi za kimataifa kuunga mkono utatuzi wa amani kwa mzozo huo.

Alisisitiza kwamba vita vitaleta tu mauaji, uharibifu na chuki zaidi duniani. El-Tayyeb aliongeza kuwa tofauti zinaweza kutatuliwa tu kupitia mazungumzo. Viongozi wengi wa dunia wakiwemo viongozi wa kidini wamezitaka Moscow na Kiev kutatua masuala yao kidiplomasia.

Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Alhamisi alitangaza kuanzisha operesheni za kijeshi Ukraine kuondoa kile alichokiita tishio kubwa kwa nchi yake, na kuutuhumu uongozi Ukraine kuwa unaoungwa mkono na nchi za Magharibi katika kutekeleza mauaji halaiki dhidi ya wanaozungumza Kirusi mashariki mwa Ukraine.

Alisema lengo la operesheni hiyo ni kuiondoa Ukraine katika hali ya kijeshi na kwamba hana nia ya kuvamia ardhi ya nchi hiyo. 

Nchi za Magharibi zimetangaza vikwazo vingi dhidi ya Russia, ikiwa ni pamoja na kuorodhesha benki zake na kupiga marufuku usafirishaji wa teknolojia.

Katika Umoja wa Mataifa, Russia  ilipinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la kukashifu operesheni yake.

Wakati huo huo, Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, muungano wa kijeshi wa NATO haupaswi kuzitaja oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine kuwa ni uvamizi.

Akizungumza Jumamosi usiku, Zakharova amesema: "Kwa kuzingatia kushindwa nchi za NATO kufanya mazungumzo na kutokuwa na irada ya kuimarisha usalama wa Ulaya kwa msingi wa mlingano katika usalama, sasa zinajaribu kutoa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti Russia imeivamia Ukriane."

Zakharova amesema kabla ya nchi za  NATO kutaka Russia itoe majibu kutokana na oparesheni zake nchini Ukraine zenye lengo la kuondoa muundo wa kijeshi Ukraine, NATO inapaswa kufafanua kuhusu chokochoko zake za kijeshi. Aidha amesema NATO inapaswa kutoa jibu ni kwa nini imekataa kuushawishi utawala wa Ukraine ufuatilie njia za amani katika kutatua matatizo yaliyojitokeza.

4039027

captcha