IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ukraine imekuwa mhanga wa siasa za utawala wa kimafya wa Marekani

20:21 - March 01, 2022
Habari ID: 3474989
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani ni utawala wa kimafia na kwamba, Ukraine imekuwa mhanga wa siasa za utawala huo.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo katika hotuba ya moja kwa moja kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa maadhimisho ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume, Muhammad SAW, na kubainisha kwamba, Marekani ni mfano kamili wa ujahilia wa kisasa. Ameendelea kusema kwamba, Marekani imekuwa ikiibua na kupandikiza migogoro na Ukraine imekuwa mhanga wa siasa hizo za Washington.

Kiongozi Muadhamu amesema, Iran inapinga mauaji na uharibifu wa miundomsingi katika eneo lolote lile duniani na msimamo wake kuhusiana na matukio ya sasa ya Ukraine ni kusitishwa vita.

Akizungumzia mnasaba wa leo wa kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume SAW, Ayatullah Khamenei amesema, kutumwa Mtume Muhammad SAW,ilikuwa ni zawadi kwa jamii yote ya mwanadamu. Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa, katika zama za ujahilia jamii ya wakati huo ilikuwa na sifa ya kutenda dhulma na ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la fitina zinazotokana na taasubi za kijahilia ambapo Mtume SAW alifanikiwa kujenga umma mmoja kutoka katika jamii hiyo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tunapaswa kupata ibra na mafunzo katika kubaathiwa Mtume na miongoni mwayo ni kusimama na kukabiliana na ujahilia kupitia kuimarisha imani ya dini.

Aidha amesema, wananchi ndio waungaji mkono wakubwa wa serikali na ndio ambao utawala unapaswa kuwaamini. Ameongeza kuwa, kama wananchi wangejitokeza katika medani Ukraine isingekumbwa na hatima ya sasa. Ni kama ilivyokuwa huko Iraq ambapo Marekani ilipovamia wananchi hawakujitokeza kukabiliana na Marekani na ndio maana utawala wa dikkteta Saddam ukaanguka.

Kiongozi Muadhamu amekumbusha kwa kusema kuwa, baada ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh kuivamia Iraq wananchi walijitokeza na kupambana kwa hali na mali na kufanikiwa kulisambaratisha kundi hilo la kigaidi.

Vilevile amebainisha kwamba, Jamhuri ya kiislamu ya Iran imepitia tajiriba hii ambapo tumeona katika vita vya miaka minane licha ya dikteta Saddan kuungwa mkono na karibuni dunia nzima lakini wananchi wa Iran kutokana na kuiamini  serikali na kuwa pamoja na mfumo wa Kiislamu walijitokeza na kufanikiwa kuushinda utawala wa dikteta Saddam pamoja na washirika wake.

4039625

captcha