IQNA

Ni kwa nini Russia imeanzisha oparesheni maalumu ya kijeshi Ukraine?

15:20 - February 24, 2022
Habari ID: 3474970
TEHRAN (IQNA)- Rais Vladimir Putin wa Russia mapema Alhamisi amehutubia taifa katika televisheni na kutangaza kuwa, vikosi vya nchi yake vimeanza oparesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass ambalo limetangaza kujitenga na Ukraine. Punde baada ya kutangaza oparesheni hiyo ya kijeshi, Putin ametaka kusitishwe 'muundo wa kijeshi' Ukraine na kuitaka nchi hiyo iweke chini silaha zake.

Katika kubainisha mtazamo wa kisheria wa oparesheni hiyo ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine, Putin amesema: "Kwa mujibu wa kipengee cha 51, sura ya saba ya Hati ya Umoja wa Mataifa, na kwa idhini ya Baraza la Kifederali la Russia katika utekelezaji wa mapatano ya kirafiki na msaada kwa maeneo ya  Donetsk na Lugansk, uamuzi umechukuliwa kwa ajili ya kutekeleza oparesheni maalumu ya kijeshi." Ameongeza kuwa: "Serikali inayotawala Ukraine inabeba dhima kamili ya umwagaji wowote wa damu utakaotokea. 

Kama ilivyotarajiwa, baada ya Russia kutambua uhuru wa maeneo mawili ya Donetsk na Lugansk, yaliyotangaza kujitenga na Ukraine, maeneo hayo yamemuomba msaada Rais Putin na kwa msingi huo mapema Alhamisi 24 Februari Russia imeanza oparesheni kubwa za kijeshi nchini Ukraine kwa kudondosha mabaomu katika vituo vya kijeshi na maghala ya silaha nchini humo.

Ukraine ilipuuza tahadhari za Russia

Kwa msingi huo, baada ya indhari kadhaa za  Russia kwa Ukraine na upuuzaji wa wakuu wa Kiev kwa tahadhari hizo, sasa Russia imeamua kuchukua hatua za kivitendo. 

Rais Joe Biden wa Marekani ametoa taarifa na kusema Russia inabeba dhima ya vita vya Ukraine na maafa yatakayotokana na vita hivyo. Hii ni katika hali ambayo Marekani imekuwa na nafasi kubwa katika kuibua mgogoro wa sasa nchini Ukraine.

Tunaweza kusema kuwa, oparesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine ni mwanzo mpya katika uga wa kimataifa.

Uchokozi wa Marekani, NATO dhidi ya Russia

Katika miaka ya hivi karibuni, Russia na kambi ya Magharibi, na hasa Russia na NATO na Marrekani zimekuwa zikivutana kisiasa na kidiplomasia na vile vile zimehusika katika vita vya vyombo vya habari au kipropaganda.

Mara kadhaa Russia imeutahadharisha muungano wa kijeshi wa NATO kuhusu kujipanua na kuelekea Mashariki na kuweka vituo vyake ya kijeshi katika mipaka ya Russia.  Wakuu wa Russia wanaamini kuwa upanuzi huo wa NATO kuelekea Mashariki ni tishio kubwa kwa usalama wake.

Pamoja na hayo, NATO ikiongozwa na Marekani imekuwa ikipuuza wasiwasi wa Russia huku ikisisitiza kuwa Ukraine ijiunge na muungano huo wa kijeshi.

Kadhia nyingine muhimu ni kuwa, watawala wenye mitazamo ya Kimagharibi nchini Ukraine, hasa baada ya matukio ya kisiasa ya mwaka 2014, wakati rais mwenye mielekeo ya Russia, Viktor  Yanukovych, alipoondolewa madarakani, na ukaanza urais wa Petro Poroshenko na kisha akaingia madarakani rais wa sasa Volodymyr Zelenskyy, nchi hiyo imekuwa ikijaribu sana kujiunga na NATO.

Mnamo Februari 2019, Poroshenko alisema kuna ulazima kwa Ukraine kujiunga na NATO na Umoja wa Ulaya na hata bunge lilipitisha sheria ya mabadiliko ya katiba kufanikisha lengo hilo.

Kutegemea Marekani kumesababisha hasara

Serikali ya sasa ya Ukraine nayo badala ya kuzingatia wasiwasi wa Russia, imekuwa na dhana potovu kuwa inaweza kukabiliana na Russia kwa msaada wa NATO na Marekani. Hii ni katika hali ambayo uzoefu wa  nyuma kama vile vilta vya Georgia vya mwka 2008 unaoneysha kuwa Russia haina mzaha hata kidogo katika masuala ya usalama wake wa taifa hasa wakati wa kukabiliana na njama za Magharibi hasa NATO.

Hivi sasa pia Putin ametoa onyo kali kuwa atakabiliana kwa nguvu na upande wowote wa kigeni utakaothubutu kuingia kijeshi katika mgogoro wa Ukraine.

Kwa hakika hivi sasa serikali ya Ukraine inakumbana na matokeo ya sera zake za kusisitiza kujikurubisha kwa madola ya Magharibi na NATO sambamba na kuhasimiana na Russia. Kwa maelezo hayo, hivi sasa si tu kuwa Ukraine haijaweza kupata usalama iliodhani ingepata kwa kujikurubisha kwa NATO bali sasa pia inakabiliwa na vita haribifu sambamba na kugawanyika vipande vipande.

4038551

Kishikizo: ukraine russia Putin
captcha