Kituo cha Haki za Binadamu cha Mizan kimetoa ripoti kwa mnasaba wa Siku ya Mwanamke Ulimwenguni na kusema kuwa, wanawake 60 wa Palestina wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya Wazayuni huko Ghaza baina ya tarehe 8 Machi 2021 hadi tarehe 8 Machi 2022.
Taarifa ya kituo hicho imesema kuwa, wanawake wote hao wa Palestina wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi za kivita na wanajeshi makatili wa Israel na pia kwenye mashambulizi yanayofanywa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, wakati wa vita vya pande zote vya siku 11 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Mei 2021, wanawake 99 wa Kipalestina walipoteza waume zao na kubakia bila ya watu wa kuwahudumia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyumba 742 zilizokuwa zinamilikiwa na wanawake ziliharibiwa na Wazayuni katika vita hivyo vya pande zote vya siku 11 huko Ghaza.
Kabla ya hapo, taasisi ya mateka wa Kipalestina ilikuwa imetangaza kuwa, kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Agosti mwaka jana 2021, wanawake 130 wa Palestina walitekwa nyara na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na kupelekwa kusikojulikana.
Kwa mujibu wa Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina, wengi wa wanawake hao wa Palestina waliotekwa nyara na wanajeshi Wazayuni katika kipindi cha miezi hiyo minane, ni wakazi wa mji wa Baytul Muqaddas.
Hii ni katika hali ambayo, mwaka wa kabla yake yaani 2020, wanawake wasiopungua 128 wa Palestina walitekwa nyara na wanajeshi dhalimu wa Israel na kupelekwa kusikojulikana.