IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Siku ya Kimataifa Quds ni fursa ya kutangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina

19:18 - April 27, 2022
Habari ID: 3475173
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maadhimisho ya Siku ya Quds ni fursa ya kutangaza kuwa pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina ambapo licha ya taifa hilo kudhulumiwa lakini limepata nguvu na kuwa imara.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo alipokutana na vikundi na jumuiya za wanachuo ambapo sambamba na kuashiria jihadi na mapambano ya vijana wa Palestina ambayo hayaruhusu kadhia ya Palestina isahauliwe amesema kuwa, Siku ya Quds ni fursa mwafaka ya kutangaza kuwa pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina na kuwapa moyo.

Ayatullah Khamenei ameashiria kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kubainisha kwamba, maadhimisho ya mwaka huu ya siku hii yanatofautiana na ya miaka ya huko nyuma.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, wananchi na vijana wa Kipalestina wanaonyesha kujitolea kwao pakubwa na utawala haramu wa Israel unatumia mbinu chafu na kutenda jinai kubwa na kufanya chochote utakacho huku Marekani na madola ya ulaya yakiendelea kuunga mkono utawala huo ghasibu.

Ayatullah Khamenei amekosoa vikali utendaji wa tawala za Kiislamu kuhusiana na suala la Palestina na kusema kuwa, inasikitisha kuona kwamba, madola ya Kiislamu yamekuwa na utendaji mbaya mno na hata hayako tayari kuzungumzia kadhia ya Palestina.

Aidha amesema kuwa, baadhi ya madola ya Kiislamu yanadhani kwamba, njia ya kulisaidia taifa la Palestina ni kuanzisha uhusiano na Wazayuni katika hali ambayo kufanya hivyo ni kosa kubwa.

Kiongozi Muadhamu ameashiria kosa kubwa lililofanywa na serikali ya Misri miaka 40 iliyopita kwa kuanzisha uhusiano na Wazayuni na kuhoji kwa kusema: "Hivi kwani Misri haikuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni? Je, uhusiano huo umepunguza jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina? Je, uhusiano baina ya Misri na utawala wa Kizayuni, umeweza kupunguza kuvunjiwa heshima Msikiti wa al Aqsa? Mbona hivi sasa baadhi ya serikali za nchi za Waislamu zinataka kurejea kosa hilo hilo la Anwar Saadat?

4052798

captcha