IQNA

Ibada ya Hija

Mahujaji waanza kuwasili Madina kuashiria kuanza msimu wa Hija

15:20 - June 05, 2022
Habari ID: 3475338
TEHRAN (IQNA) – Kundi la Mahujaji kutoka Indonesia walifika Madina siku ya Jumamosi wakiwa kundi la kwanza kuwasili katika Ufalme wa Saudia kutekeleza ibada za Hija baada ya kusitishwa kwa Waislamu walio nje ya Saudia kwa muda wa miaka miwili kutokana na corona

Saudi Arabia mwezi uliopita ilitangaza kuwa itawaruhusu Waislamu milioni moja - kutoka ndani na nje ya ufalme huo - kutekeleza Hija ambayo itafanyika Julai ikilinganishwa na takriban 60,000 mwaka jana na chini ya 1,000 mnamo 2020.

"Leo tumepokea kundi la kwanza la Mahujaji wa mwaka huu kutoka Indonesia, na safari za ndege zitaendelea kutoka Malaysia na India," Mohammed al-Bijawi wa Wizara ya Hija ya nchi hiyo amesema.

"Leo tunafuraha kuwapokea wageni wa Mwenyezi Mungu kutoka nje ya ufalme, baada ya kukatizwa kwa miaka miwili kutokana na janga hili," aliongeza, na kuendelea kusema kwamba Saudi Arabia "imejiandaa kikamilifu" kuwahudumia.

Kawaida Hija ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini ulimwenguni, takriban watu milioni 2.5 walishiriki mnamo 2019 – ambayo ilikuwa Hija ya mwisho kabla ya kuzuka janga la corona.

Kuzuia mahujaji wa ng'ambo kulisababisha masikitiko makubwa miongoni mwa Waislamu duniani kote, ambao kwa kawaida huweka akiba kwa miaka mingi ili kushiriki katika Ibada ya Hija.

Hajj ina mfululizo wa amali za Kiislamu ambazo hukamilishwa kwa muda wa siku tano katika mji mtakatifu wa Kiislamu, Makka, na maeneo ya jirani ya magharibi mwa Saudi Arabia.

Saudi Arabia hupata pato kubwa sana kutokana na Ibada ya Hija ambapo kabla ya janga la corona ilikuwa inapata karibu $ 12bn kila mwaka.

Hija ya mwaka huu itakuwa tu kwa Waislamu walio na chanjo kamili ya corona na walio chini ya umri wa miaka 65, Wizara ya Hija imesema.

Wale wanaotoka nje ya Saudi Arabia, ambao wanapaswa kutuma maombi ya visa vya Hija na wanatakiwa kuwasilisha matokeo hasi ya COVID-19 PCR kutokana na jaribio lililochukuliwa ndani ya saa 72 za kusafiri.

3479174

captcha