IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuanza tena ibada ya Hija ni baraka kubwa kwani ibada hii ni nembo ya umoja wa Waislamu

18:29 - June 08, 2022
Habari ID: 3475348
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua ya kuanza tena ibada ya Hija baada ya amali hiyo kuvurugwa kwa miaka miwili na janga la Corona. Amesema, "hii ni baraka kubwa kwani ibada hii ni nembo ya umoja miongoni mwa Waislamu."

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo Jumatano hapa mjini Tehran katika hotuba yake mbele ya maafisa wanaosimamia masuala ya Hija wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ameikumbusha Saudi Arabia kuwa mji mtukufu wa Makka ni milki ya Waislamu wote, na serikali ya Riyadh inapaswa kufanya mambo kwa kuzingatia matakwa ya ulimwengu wa Kiislamu, na si matakwa yake tu. Ameitaka Saudia kulinda usalama wa Mahujaji ili kuzuia kutokea mikasa na majanga kama yaliyoshuhudiwa huko nyuma.

Ayatullah Ali Khamenei kadhalika ametoa mwito wa kufanywa jitihada za kuhakikisha kuwa umoja wa Waislamu unadumishwa na kuonya kuwa, kuibua mifarakano na mipasuko kwa misingi ya madhehebu ni njama ya muda mrefu inayotumiwa na Uingereza.

Amefafanua kuwa, "matatizo wanayokumbana nayo wanadamu duniani hii leo, si Waislamu tu, yamesababishwa na watu kushindwa kuishi pamoja kwa amani, huku wakidhulumiana na kuumizana." 

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema tawala za Kiarabu zilizokhitari kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel bila ridhaa ya wananchi wao hazitakumbwa na hatima nyingine ghairi ya kuishia kudhalilishwa na kutumiwa vibaya na utawala huo haramu.

Ayatullah Ali Khamenei amebainisha kuwa, "kufichua njama za utawala wa Kizayuni ni moja ya majukumu makuu ya ibada tukufu ya Hija."

Ameeleza bayana kuwa: Madola ya Kiarabu na yasiyokuwa ya Kiarabu yaliyoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni bila ridhaa ya wananchi lakini kwa kufuata matakwa ya Marekani, yanapaswa kuelewa kuwa, mahusiano haya hayatakuwa na matokeo mengine isipokuwa kufanyiwa idhilali na kutumiwa vibaya na utawala wa Kizayuni.

4062741

captcha