IQNA

Iran yalalamikia vikali kauli za kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW nchini India

10:41 - June 06, 2022
Habari ID: 3475340
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa India mjini Tehran kulalamikia vikali matamshi dhidi ya Mtume Mutukufu wa Uislamu, Muhammad SAW ambayo yalitolewa katika mdahalo wa televisheni huko India na kuibua hasira miongoni mwa Waislamu duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Asia Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumapili alimuita Balozi wa India ili kubainisha malalmiko makali ya serikali na watu wa Iran kuhusu matamshi yaliyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Kwa upande wake, Balozi wa India alibainisha masikitikio yake kuhusiana na kadhia hiyo huku akisisitiza kuwa, kitendo chochote kile cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW hakikubaliki.

Balozi huyo aidha alibainisha wazi kuwa matamshi hayo yaliyotolewa na maafisa wawili wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) hayawakilishi msimamo wa serikali ya India ambayo inaheshimu dini zote.

Katika matamshi ya hivi karibuni katika mdahalo wa televisheni, msemaji wa BJP Nupur Sharma alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Mtume wa Uislamu, ambayo yamelaaniwa kote India na kuibua ghasia katika jimbo la Uttar Pradesh Kanpur siku ya Ijumaa. Jana Jumapili chama cha BJP kilitangaza kusimamisha uanachama wa Sharma na kujiweka mbali na matamshi yake yenye chuki.

Aidha chama hicho kimemfukuza Naveen Kumar Jindal ambaye anasismamia kitengo cha habari cha chama hicho mjini New Delhi ambaye alituma ujumbe uliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katika ukurasa wake wa Twitter na kufuatia malalamiko alifuta ujumbe huo.

Nchi zingine za Kiislamu ambazo zimelaani kauli za kumvunjia heshima Mtume SAW nchini India ni Qatar, Kuwait na Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC).

3479181

captcha