IQNA

Imam Ridha AS na umaarufu wa elimu yake

12:31 - June 11, 2022
Habari ID: 3475362
TEHRAN (IQNA)- Leo mji mtakatifu wa Mashhad umetanda furaha katika haram ya Ali bin Musa Ridha AS iliyoko katika mji wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran.

Siku kama ya leo miaka 1295 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaada mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha AS, mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad AS katika mji wa Madina.

Idadi kubwa ya waumini wamefika katika haram hiyo kwa ajili ya kujumuika katika siku hii ya furaha ya kukumbuka kuzaliwa Imam Ali bin Musa Ridha AS ambaye ni kutoka katika kizazi kilichotakasika cha Mtume Muhammad SAW.

Imamu huyo mkarimu ambaye alikuwa mbeba bendera ya Wilaya, katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka aliufungulia Umma milango ya hekima na maarifa na hivyo akawa kigezo cha ucha Mungu na ubora kwa lengo la kufikia saada.

Imam Ridha AS aliishi sehemu ya maisha yake katika zama za utawala wa Ma'amun, khalifa wa silisili ya Bani Abbas. Ma'amun alikuwa mtu mwenye ujanja wa kisiasa na hila na alijiarifisha kama mtu apendaye elimu.

Vikao vya kielimu na wasomi

Mara kwa mara alikuwa akiandaa vikao vya kielimu vilivyohudhuriwa na Imam Ridha AS na wasomi wengine wa kidini na kimadhehebu ili wafanye midahalo.

Lengo la Ma’amun lilikuwa ni kutia dosari shakhsia ya kielimu ya Imam. Lakini kinyume na alivyotarajia Ma’amun, vikao hivyo vilipelekea shakhsia iliyojaa fadhila na elimu ya Imam Ridha AS kubainika wazi kwa wote. Hii ni kwa sababu Imam Ridha AS alijibu kikamilifu maswali yote aliyoulizwa katika nyanja mbali mbali za kielimu. Ujuzi mkubwa na elimu ya hali ya juu ya Imam ni jambo ambalo lilipelekea Ma’amun kukiri kuwa: “Hakuna mtu mwenye ujuzi mkubwa duniani kumliko Hadhrat Ridha.”

Imam Ridha AS alibainisha moja ya sifa muhimu za Imamu kwa kusema Imamu anatakiwa kuwa na elimu na uono wa mbali au hekima. Imam Ridha AS amenukuliwa akisema: “Elimu na ujuzi wa Imam daima huwa unastawi, huwa ni mpole, mwenye kufahamu kikamilifu masuala ya kisiasa na huwa ni mwenye kustahiki uongozi. Imam ni mlinzi wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuwalingania watu kwa hekima, mawaidha, uzuri na hoja za wazi ili waelekee katika njia ya Mwenyezi Mungu.”

Kuhuisha Uislamu

Imam Ridha AS kwa kuzingatia kikamilifu matukio ya kielimu na kisiasa ya zama, alitekeleza ipasavyo risala yake kwa lengo la kuhuisha Uislamu wa kweli na kuwaongoza wanaadamu katika njia ya haki. Kwa kutumia fikra zake za Uislamu halisi, mtukufu huyo aliwaondoa wanaadamu kutoka njia potofu na kuwaongoza katika njia iliyonyooka. Kwa hakika Imam Ridha AS alikuwa mfano wa daraja la mawasiliano baina ya waja na Allah SWT na hivyo kuwafanya waweze kufahamu kwa kina mafundisho yenye thamani ya Kiislamu. Daima mtukufu huyo alikuwa akitoa wito kwa watu kutafakari na kuwa na tadbiri katika dini kwa kusema: “Ibada si kufunga na kuswali kwa wingi bali ibada (ya kweli) ni kutafakari sana kumhusu Allah SWT.”

Miongoni mwa Maimamu waliotakasika, Imam Ridha AS alipata lakabu ya “Alim Aali Mohammad” yaani  ‘Msomi wa Kizazi cha Mohammad.'

Hali bora zaidi kwa mwanaadamu ni kunyenyekea na kuwa na khushuu mbele ya Allah SWT. Kuhusu hili Imam Ridha AS alisema: “Hali ya kuwa karibu zaidi mja na Allah SWT ni katika hali ya kusujudu na hili linaenda sambamba na ile kauli ya Allah Tabaraka wa Ta’ala aliposema:  ‘Sujudu ili ukaribie.”

Sifa za uhakika wa Imani

Ali bin Musa Ridha AS katika hadithi anasema hivi: “Hakuna mja anayefikia uhakika wa imani isipokuwa awe na sifa tatu: Maarifa na ufahamu katika dini, msimamo wa wastani katika maisha na subira katika misiba.”

Kimsingi ni kuwa mwanaadamu hufikia imani kamili anapokuwa na maarifa kamili, khushuu na kutekeleza faradhi za kidini kwa uono wa mbali. Katika utumizi wa fedha katika maisha vile vile hapaswi kuwa na misimamo ya kufurutu mipaka na katika matatizo ya maisha Mwislamu anapaswa kuwa mstahamilivu na kukubali takdiri ya Mwenyezi Mungu.

Katika zama za khalifa wa Bani Abbas, Ma’amun baadhi ya wakati alikuwa akiwaita wasomi wa taaluma ya tiba kutoka maeneo mbali mbali kwa lengo la kufanya midahalo ya kisayansi ili kwa njia hiyo aweze kupata itibari.

Katika moja ya vikao hivyo vya kisayansi alihudhuria Imam Ridha AS na Ma’amun ambapo kundi la matabibu na wanafalsafa maarufu wa Nishabur walihudhuria. Walitoa hotuba nyingi kuhusu masuala ya kitiba. Imam Ridha AS alikaa kimya na kutosema chochote. Ma’amun alumwambia hivi Imam Ridha AS: "Ya Abal Hassan! Una nini cha kusema kuhusu maudhui hizi?"

Siri ya tiba ya Imam Ridha

Imam alisema: “Nina maoni ambayo usahihi wake nimeupata kupitia tajriba ya muda mrefu. Zaidi ya hayo nina elimu ambayo waliotangulia waliniachia na kuna mambo ambayo kila mwanaadamu anapaswa kuyajua. Nitakusanya nadharia hizi na tajriba pamoja na yote yanayohitajika katika uga huu.”

Imam alitayarisha risala yake na kumkabidhi Ma’amun. Ili kuonyesha umuhimu wa risala hiyo, Ma’amun aliamuru iandikwe kwa wino wa dhahabu na ihifadhiwe katika hazina ya serikali. Ni kwa sababu hii ndio ikapewa jinal la “Risalatul Dhahabiyya.” Hivi ndivyo mjumuiko huu wa maelezo ya kitiba ya Imam Ridha AS kuhusu afya ya mwili ulikusanywa katika risala hiyo iliyopewa jina la Dhahabiyya. Katika risala hii Imam amesherehesha faida za vyakula mbali mbali, mbinu za kitiba na kiafya pamoja na namna ya kukabiliana na maradhi ya kiroho na kinafasi.

Risala hii imejaa siri nyingi. Katika risala hii Imam ameandika hivi: “Mwenyezi Mungu hajaufanya mwili uwe na ugonjwa isipokuwa ameujaalia uwe na dawa ya kutibu…”

Katika sehemu ya kitabu hicho chenye thamani ambacho pia ni maarufu kama ‘Tibb Ar Ridha’, Imam Ridha AS amesema: “Iwapo watu wataridhika kula chakula kichache, miili yao itakuwa na mlingano.”

Risala hii ya tiba iliyojaa balagha ni kati ya vitabu vyenye thamani kubwa vya Kiislamu katika uga wa tiba. Kitabu hicho kimebainisha maudhui mbali mbali za kitiba kama vile biolojia, fiziolojia, kemia, lishe n.k. Kitabu hiki kinamuongoza mwanaadamu katika maisha bora yenye afya ambayo ni neema kubwa ya Allah SWT.

 

Kishikizo: imam ridha as tiba elimu
captcha