IQNA

Mapambano dhidi ya Israel

Harakati ya Jihad Islami kuendeleza mapambano hadi Ukombozi Kamili wa Palestina

17:25 - August 17, 2022
Habari ID: 3475637
TEHRAN (IQNA) - Afisa wa harakati ya mapambano ya Jihad Islami ya Palestina anasema mapambano na muqawama dhidi ya utawala vamizi na ghasibu wa Israel yataendelea hadi ukombozi wa ardhi zote za Palestina.

"Harakati ya Jihad ya Palestina itaendelea na mapambano," mwakilishi wa harakati hiyo nchini Iran Nasser Abu-Sharif alisema siku ya Jumatano, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Khaled al-Qaddumi, mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, nchini Iran, kuhusu mafanikio ya vita vya hivi punde kati ya Israel na harakati za muqawama na mapamabano ya ukombozi katika Ukanda wa Gaza.

"Lengo kuu halijafikiwa, na mapambano haya yataendelea hadi ukombozi kamili wa ardhi ya Palestina," alisema.

Abu-Sharif alibainisha kuwa kuuawa shahidi sio kikwazo kwa ukombozi wa ardhi ya Palestina.

Amesema namna muqawama na taifa la Palestina linavyojibu utawala wa Israel imebadilika katika miaka ya karibuni.

"Ni kweli kwamba tulipoteza makamanda wetu wawili waandamizi, Khaled al-Mansour na Tayseer al-Jabari, na hii ni hasara kubwa, lakini harakati ya Jihad ya Kiislami ya Palestina ni harakati iliyopangwa ambayo inaweza kuchukua nafasi ya makamanda hawa waliouawa shahidi," aliongeza.

Abu-Sharif alikuwa akiashiria wimbi la mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yaliyoanza tarehe 5 Agosti na kudumu kwa siku tatu mfululizo, na kuua makumi ya watu, wakiwemo watoto 17 na wanachama wakuu wa Jihad Islami na  mamia wengine pia walijeruhiwa wakati wa uvamizi wa Israel.

Katika kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, Jihad Islami ilivurumisha mamia ya makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, na kuufanya utawala wa Tel Aviv kukubali usitishaji vita uliosimamiwa na Misri.

"Harakati za muqawama zitalipiza kisasi damu ya mashahidi wa Kipalestina"

Qaddumi kwa upande wake alisema harakati za muqawama au mapambano zitalipiza kisasi cha damu ya mashahidi wa Kipalestina. Aliwataka waandishi wa habari kuripoti ukatili wa utawala wa Israel.

"Katika uvamizi wake dhidi ya Ukanda wa Gaza, utawala wa Kizayuni uliua shahidi idadi ya raia wa Palestina, wakiwemo watoto watano katika kambi ya Jabalya," alisema.

Israel siku ya Jumanne ilikiri kwamba ilihusika na mauaji ya watoto hao watano wa Gaza huko Jabalya, baada ya awali kulaumu maroketi ya Jihad Islami kuwa yalipoteza mwelekeo na kulenga watoto hao.

"Tulizungumza na ndugu zetu mwanzoni mwa vita vya hivi majuzi ili kukabiliana na uhalifu huu," Qaddumi alisema. “Tulizungumzia mambo mawili kwa wakati mmoja. Kwanza, utawala wa Kizayuni unawajibika kwa jinai yoyote ile, na pili, tuna haki ya kujibu kihalali jinai hizo na kulipiza kisasi.”

Mwakilishi huyo wa Hamas amesema utawala wa Israel ulianzisha vita vya kipropaganda dhidi ya muqawama katikati ya vita hivyo na kudai kuwa makundi ya muqawama ya Palestina hayakuwa na umoja.

"Tuko katika wakati mgumu sana kuhusu suala la Palestina na tunatoa pongezi zetu kwa ushindi katika vita vya hivi karibuni vya Gaza, ambavyo vilizua kizuizi dhidi ya wavamizi," aliongeza.

3480135

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha