IQNA

Kombe la Dunia la Qatar

Mashabiki wa Kombe la Dunia wajifunza kuhusu Uislamu katika Msikiti wa Doha

20:08 - November 24, 2022
Habari ID: 3476139
TEHRAN (IQNA) – Wahubiri wa kiume na wa kike wenye uwezo wa kuzungumza lugha kadhaa katika Msikiti wa Kijiji cha Utamaduni cha Katara katika mji mkuu wa Qatar wa Doha wanatoa maelezo kuhusu Uislamu na halikadhalika wanabainisha uvumilivu wa dini hii tukufu kwa watalii wakati wa Kombe la Dunia la 2022.

Msikiti huo umekuwa kitovu cha mashabiki wa Kombe la Dunia wanaotaka kujua kuhusu Uislamu.

Mabango ya kielektroniki kuhusu Uislamu katika lugha zaidi ya 30 mlangoni ambapo kuna maelezo ya kuwawezesha  wageni kutumia simu zao za mkononi kuujua Uislamu.

Aidha vijitabu vinavyotambulisha Uislamu katika lugha tofauti husambazwa kwa wale wanaovitaka.

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu nchini Qatar pia imezindua banda la kutambulisha Uislamu na mafundisho yake wakati wa Kombe la Dunia 2022.

Mashabiki wa Kombe la Dunia hukutana na hadithi - maneno, vitendo, au tabia za Mtume Muhammad (SAW) – kwenye maandishi katika kuta za barabara, zinazoelezea umuhimu wa matendo mema.

Sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia la FIFA 2022 zilifanyika Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Al Bayt mjini Al Khor, ambapo usomaji wa aya za Qur'ani Tukufu na Ghanim Al Muftah, mwenye umri wa miaka 20, pia balozi wa FIFA wa Kombe la Dunia, ulisisimua sana watazamaji duniani kote.

Hafla hiyo katika uwanja wa umbo la hema ilifanyika kabla ya mechi ya kwanza kati ya wenyeji Qatar na Ecuador.

Ikiwa nchi ndogo zaidi kuwahi kuandaa tukio kubwa zaidi la soka duniani, Qatar, ni nchi tajiri ya Ghuba ya Uajemi ambayo ni mzalishaji mkubwa wa gesi. Qatar imetumia vizuri fursa iliyojitokeza ya Kombe la Dunia kuarifisha dini tukufu ya Kiislamu kwa wageni waliofika nchini humo.

3481384

Kishikizo: qatar ، kombe la dunia ، uislamu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha