IQNA

Kombe la Dunia la Qatar

Qatar yazindua Kombe la Dunia la FIFA 2022 kwa aya ya Qur’ani Tukufu

23:26 - November 21, 2022
Habari ID: 3476127
TEHRAN (IQNA) - Kombe la Dunia la FIFA la 2022 nchini Qatar lilianza Novemba 20 kwa usomaji wa aya ya Qur’ani Tukufu na yamkini hii ni mara ya kwanza katika historia ya kombe hilo.

Aidha mizizi ya Bedui ya Qatar ilionyeshwa wakati wa sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia.

Wakati Emir wa nchi hiyo akifungua Kombe la Dunia, alibusu mkono wa babake na kukaribisha ulimwengu kwenye hafla kubwa zaidi ya kandanda, ikiwa ni mara ya kwanza kuandaliwa na nchi ya Asia Magharibi ua Mashariki ya Kati.

"Hapa  Qatar na hapa katika ulimwengu wa Kiarabu, ninamkaribisha kila mtu kwenye Kombe la Dunia la 2022," Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani alisema. "Inapendeza sana kwamba watu wanaweza kuweka kando kile kinachowagawanya kusherehekea utofauti wao na kile kinachowaleta pamoja." Kisha, fataki zililipuka kutoka kwa paa la uwanja wa Al Bayt.

Lakini kilichouteka ulimwengu na kuwavutia watazamaji ni kusomwa aya za Qur'ani Tukufu na msomaji wa Qur'ani mwenye umri wa miaka 20 Ghanim Al Muftah, ambaye pia ni balozi wa FIFA wa Kombe la Dunia.

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane.Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi.” ilisema sehemu ya aya ya 13 ya Sura al Hujuraat aliyoisoma Ghanim. Inaaminika hii ni mara ya kwanza kwa Kombe la Dunia la FIFA kufunguliwa kwa aya za Qur’ani

Ghanim, aliyezaliwa na hali ya nadra ambayo inadhoofisha ukuaji wa upande wa chini wa mwili, alionekana pamoja na mwigizaji mshindi wa Oscar Morgan Freeman. Muigizaji huyo wa Kimarekani alikaa uwanjani kando ya msomaji Qur’ani (qari) huyo wa Qatari.

Freeman alisimulia sehemu ya ufunguzi wa hafla ya ufunguzi wa Kombe la Dunia la 2022, iliyopewa jina la 'Wito', akiwaambia watazamaji: 'Sote tunakusanyika hapa kama kabila moja kubwa'.

"Nchi nyingi, lugha na tamaduni zinawezaje kukusanyika ikiwa njia moja tu itakubaliwa?" Freeman aliuambia umati.

"Unapofika  hapa, tunakukaribisha nyumbani kwetu," Ghanim alisema, akirejelea 'bayt al sha'ar' au hema ambalo Mabedui wahamaji wa Rasi ya Uarabuni walitumia wakati mmoja kama makazi. Muundano wa hema hilo ndio uliotegemewa na wajenzi wa uwanja huo wa sherehe za ufunguzi.

"Nilisikia kitu kizuri. Sio muziki tu, bali pia wito huu  wa kukaribisha kwenye sherehe," mwigizaji huo Mmarekani mwenye asili ya Afrika alisema.

Freeman baadaye alihutubia umati, akisema, "Kandanda iliunganisha mataifa na upendo wao kwa mchezo huu mzuri. Kinacholeta pamoja mataifa pia huleta pamoja jamii."

captcha