IQNA

Jinai za Isarel

Wapalestina 70 wamefariki katika jela za Israel baada ya kunyimwa huduma za kiafya

13:10 - December 22, 2022
Habari ID: 3476287
TEHRAN (IQNA) - Takriban Wapalestina 74 waliokuwa wakishikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel wamekufa shahidi kutokana na kunyimwa huduma kiafya.

Wa kwanza alikuwa Khalil Al-Rashaida kutoka Beit Lahm (Bethlehem), ambaye alifariki mwaka 1968 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo na hakupewa matibabu yanayohitajika.

Mwathiriwa wa hivi punde, aliyefariki Jumanne, alikuwa Nasser Abu Hamid, kutoka kambi ya Al-Amari. Alitangazwa kufariki kutokana na  saratani baada ya huduma za magereza ya Israel kukataa kumpa matibabi kwa wakati.

Mahakama ya utawala dhalimu wa Israel ilikataa ombi la kuachiliwa kwake mapema kwa sababu ya kuzorota kwa afya yake.

Kulingana na Jumuiya ya Wafungwa wa Palestina, takriban wafungwa 600 wagonjwa wanazuiliwa katika jela za kuogofya za utawala vamizi wa Israel, wakiwemo takriban 200 wanaougua magonjwa sugu. Hii inajumuisha wafungwa 24 wenye uvimbe na saratani.

Saadia Farajallah, 68, alifariki Julai kutokana na uzembe wa kimakusudi wa kimatibabu. Aliugua kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya moyo. Alikuwa amefika mahakamani akiwa kwenye kiti cha magurudumu siku chache kabla ya kifo chake, hii ilitokana na kuzorota kwa afya yake.

Hamas yatoa taarifa

Wakati huo huo, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Palestina, Hamas, amelaani kifo cha mfungwa wa Kipalestina aliyekuwa anaugua kansa katika jela za Israel na kusema kuwa jinai za utawala huo hazitapita bila kuadhibiwa.

Ismail Haniyah aliyasema hayo katika taarifa siku ya Jumanne, baada ya Nasser Abu Hamid, ambaye alikuwa anasumbuliwa na hali ya kiafya ya kutishia maisha katika mapafu yake akiwa kizuizini Israel, kutangazwa kuaga dunia na Tume ya Wafungwa wa Palestina mapema hapo jana.

Ismail Hania ametuma salamu za rambirambi za dhati kufuatia kifo cha Abu Hamid kwa mama yake na ndugu zake waliowekwa kizuizini katika jela za utawala haramu wa Israel na kusisitiza dhamira ya harakati hiyo ya kuwakomboa wafungwa wote wa Kipalestina wanaoteseka katika jela za utawala huo wa kibaguzi.

Abu Hamid alitangazwa kufariki dunia Jumanne asubuhi katika Kituo cha Matibabu cha Shamir cha Israeli, kilichoko kilomita 15 (maili 9.3) kusini mashariki mwa Tel Aviv.

Alihamishwa kutoka Hospitali ya Gereza ya Ramla hadi kituo hicho cha matibabu Jumatatu alasiri baada ya hali yake ya afya kuzorota na kuingia kwenye koma.

Abu Hamid aligunduliwa kuwa na saratani mnamo Agosti 2021.

Mfungwa huyo wa Kipalestina aliyekuwaumri wa miaka 50 alikuwa akikabiliwa na hali ngumu ya afya huku magereza ya Israel (IPS) yakimnyima huduma muhimu za matibabu.

Israel itafikishwa ICC

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina, Riyad al-Maliki, amesema utawala wa Israel unahusika moja kwa moja na kifo cha Abu Hamid, na kusisitiza kuwa kesi yake itawasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Maliki pia ameishutumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kushughulikia suala la Abu Hamid kwa wakati unaofaa, akisema sio tu kwamba ni mwathirika wa ukandamizaji wa utawala ghasibu wa Israel, bali pia ni mwathirika wa undumakuwili wa kimataifa.

Aidha ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa kibaguzi wa Israel ukabidhi mwili wa mfungwa huyo wa Kipalestina kwa familia yake, ili imzike haraka iwezekanavyo.

3481777

captcha