IQNA

Harakati za Qur'ani

Waziri Mkuu wa Malaysia atetea bajeti ya dola milioni 2.2 ya usambazaji nakala za Qur’ani

22:46 - February 27, 2023
Habari ID: 3476634
TEHRAN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Malaysia ametetea mpango uliopendekezwa wa kuchapisha nakala milioni 1 za Qur'ani Tukufu kwa lengo la kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu.

Takriban dola milioni 2.2 zilizotengwa chini ya Bajeti ya 2023 kwa ajili tarjuma ya   Qur’ani Tukufu kwa lugha mbali mbali na kusambaza nakala zilizochapishwa duniani kote ni kusaidia kujenga uelewa wa kina wa Uislamu na kushughulikia chuki dhidi ya Uislamu, amesema Waziri Mkuu Anwar Ibrahim.

Moja ya sababu za chuki dhidi ya Uislamu  au Islamophobia ni ukosefu wa uelewa, aliongeza.

“Kwa nini watu wanasema bajeti hii ni kubwa? ... Ni lazima tuwafanye watu wasome Qur’ani Tukufu na tarjuma au tafsiri yake ili tuweze kuelewa dini na kuuokoa Uislamu mkabala wa chuki dhidi Uislamu,” alisema baada ya kutoa hotuba kuu katika Jukwaa la Kimataifa Kuhusu Chuki Dhidi ya Uislamu mjini Kuala Lumpur Jumatatu (Feb 27).

Anwar alisema kuwa ingawa kulikuwa na pande zinazotilia shaka matumizi haya, aliamini mpango huu utawanufaisha Wamalaysia pia.

"Kwa uelewa wa kina na sahihi, hakutakuwa na mgongano wa itikadi, hakuna migawanyiko, hakuna misimamo mikali wala vurugu," aliongeza.

Wakati wa kuwasilishwa kwa Bajeti iliyorekebishwa ya 2023 mnamo Ijumaa (Feb 24), Anwar, ambaye pia ni Waziri wa Fedha, alisema takribani dola milioni 2.2 zitatengwa kutafsiri na kusambaza nakala za Qur’ani Tukufu katika lugha ya Kiswidi na lugha zingine za kigeni.

Hatua hiyo imekuja baada ya kushuhudiwa vitendo viovu vya kuteketeza nakala  za Qur’ani Tukufu nchini Uswidi na maeneo mengine ya Ulaya.

3482636

Kishikizo: qurani tukufu uislamu
captcha