IQNA

Wanamichezo Waislamu

Mwanasoka Mwislamu wa Bosnia asema mwezi wa Ramadhani unaleta jamii pamoja

14:13 - March 27, 2023
Habari ID: 3476768
TEHRAN (IQNA) - Mchezaji soka maarufu wa Bosnia na Herzegovina Anel Ahmedhodzic ameusifu mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni mwezi wa kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuleta jamii pamoja.

Beki huyo wa Sheffield United, ambaye sasa yuko katika kambi ya timu ya taifa ya Bosnia na Herzegovina, anasema ataendelea kucheza sambamba na kufunga katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Ahmedhodzic ni mzaliwa wa Uswidi kwa sababu familia yake ilihamia huko kufuatia Vita vya Balkan. Uislamu umekuwa msingi wa maisha yake tangu alipokuwa kijana huko Rosengard; eneo la Malmo ambalo kwa muda mrefu limekuwa kivutio cha wahamiaji katika nchi ya Skandinavia.

Akielezea matukio karibu na futari, wakati wale wanaofuata mafundisho ya Uislamu wanapofungua mfungo wao wa kila siku baada ya jua kutua, amesema: “Ni mwezi mtukufu. Ni mwezi wa kumwabudu Mungu na kuwa na imani thabiti. Ni mwezi ambao tunafunga kila siku hadi jua linapozama. Kwangu mimi, tangu nikiwa mtoto, marafiki zangu wote, kila mtu alikuwa akifunga na kwenda msikitini na kuswali.

"Ramadhani inaleta jamii nzima pamoja. Unaalika marafiki kwa ajili ya chakula cha jioni wakati wa Magharibi jua linapotua," aliongeza.

Saumu ya Ramadhani ambayo humuwajibisha muumini kujiepusha na chakula na vinywaji wakati wa mchana kunatajwa kuuelekeza moyo mbali na shughuli za kidunia na kuitakasa nafsi kwa kuiondoa kutoka katika uchafu unaodhuru. Mwezi wa Ramadhani pia ni wakati ambao Waislamu wanahimizwa kuwa wakarimu na kuwasaidia watu wasiojiweza Katika mwezi huu pia Zakat – ambayo ni sadaka ya wajibu – ina mchango mkubwa katika kuondoa matatizo katika jamii.

Sikukuu ya Idul Fitr, ambayo kwa kawaida huadhimishwa kwa muda wa siku tatu, huashiriamwisho wa Ramadhani. Marafiki na familia hukusanyika pamoja kwa sherehe na mapumziko.

3482955

captcha