IQNA

Jeshi katili la Israel lateka meli ya msaada iliyokuwa ikielekea Gaza

16:16 - July 27, 2025
Habari ID: 3481010
IQNA-Jeshi la majini la utawala ghasibu wa Israel limeiteka meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Ukanda wa Gaza, ikiwa na bendera ya Uingereza, katika harakati za kuvunja mzingiro mkali wa eneo hilo unaoendelea tangu mwaka 2007.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel vilivyoripoti Jumamosi, meli hiyo iitwayo Handala iliondoka nchini Italia ikiwa na watu 21 wasio na silaha wakiwemo wabunge, wahudumu wa afya, na wajitolea, wakielekea katika ukanda huo wa pwani.

Wafanyakazi wa meli waliripoti kuona ndege isiyo na rubani ikizunguka juu ya meli kabla ya kukaribiwa na meli za kijeshi za Israel. Walitoa mwito wa dharura walipojikuta katika hali ya hatari.

Huwaida Araf, mmoja wa waliokuwa ndani ya meli, alisema kuwa baada ya kuona meli za Israel, walijaribu kuwasiliana na Jeshi la Majini la Israel lakini hawakupokea majibu yoyote.

Hatimaye, Emma Fourreau, mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Ufaransa aliyekuwa ndani ya Handala, alithibitisha kutekwa kwa meli hiyo kwa kusema: “Jeshi la Israel liko hapa.”

Picha za moja kwa moja mtandaoni zilionyesha wafanyakazi wa meli wakiwa wamevaa jaketi za kujiokoa na kuinua mikono yao juu kwa tahadhari, wakijaribu kuepuka makabiliano.

“Sitisheni mauaji ya kimbari,” aliongeza Fourreau, akirejelea vita vya Israel dhidi ya Gaza vilivyoanza Oktoba 2023 na kuendelea hadi sasa.

Vita hivyo vimeshuhudia utawala wa Israel ukizidisha mzingiro wake mkali wa eneo hilo, na kuzuia karibu kabisa kuingia kwa misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa dharura. Mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja pamoja na vikwazo vilivyoongezwa—ambavyo vimekosolewa kuwa ni mbinu ya kutumia njaa kama silaha—vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 59,700, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Handala ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu ikiwemo maziwa ya watoto, chakula, na dawa, ikielekea Gaza katika hali ya mateso yasiyovumilika.

Mwezi uliopita, jeshi la Israel pia liliteka meli nyingine ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza ikiwa na wanaharakati 12 mashuhuri wa kimataifa.

Mnamo Mei, ndege zisizo na rubani za Israel zilishambulia meli nyingine iliyokuwa imebeba mwanaharakati maarufu wa Uswidi, Greta Thunberg, na wengine, karibu na pwani ya Mata.

Waangalizi wa kimataifa wanasema mashambulizi haya yanaonesha utayari wa utawala wa Israel kutumia nguvu za kijeshi kuzuia Wapalestina wa Gaza kupata misaada muhimu—hali iliyoshuhudiwa pia mwaka 2010 wakati wa shambulizi la kifo dhidi ya meli ya misaada iliyokuwa na bendera ya Uturuki.

3494006

Habari zinazohusiana
captcha