IQNA

Ufaransa yakosolewa kwa kuwazuia wachezaji Waislamu kufunga Ramadhani

8:40 - March 04, 2025
Habari ID: 3480302
IQNA – Wachezaji wa soka Waislamu nchini Ufaransa wamepigwa marufuku kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wanapokuwa wakifanya mazoezi na timu ya taifa.

Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) limeanzisha marufuku hiyo, hali iliyozua shutuma za ubaguzi na kuleta mgawanyiko ndani ya timu.

Taarifa zinasema shirikisho hilo limewaambia wachezaji wanaofunga suamu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa hawawezi kufunga wakiwa katika kambi ya mazoezi ya Clairefontaine. Badala yake, wanaweza kufidia siku zao za kufunga baada ya kumalizika kwa mechi za kimataifa.

"Marufuku ya hijabu kwa wanawake, na sasa marufuku ya kufunga kwa wachezaji wanaofunga Ramadhani. Ufaransa inaendelea kuwa bingwa wa sera za chuki dhidi ya Waislamu," alisema mwandishi wa habari za michezo wa Kanada, Shireen Ahmed, kupitia mtandao wa X (Twitter).

Wachezaji wengi wa Les Bleus wenye asili ya ya Afrika, wakiwemo Ousmane Dembélé, N’Golo Kanté, Elias Guendouzi, Ibrahima Konaté, na Ferland Mendy. Mwaka jana, kiungo chipukizi Mahamadou Diawara alijiondoa katika kikosi cha wachezaji wa chini ya miaka 19 kwa kupinga marufuku hiyo, kulingana na taarifa ya ESPN.

"Wanaamini kuwa dini yao haithaminiwi na wao wenyewe pia hawaheshimiwi," alisema wakala mmoja wa wachezaji.

Rais wa FFF, Philippe Diallo, alitetea uamuzi huo akiiambia Le Figaro:
"Hakuna mtu anayelengwa kwa ubaguzi... Lakini unapokuwa kwenye timu ya taifa ya Ufaransa, ni lazima uheshimu mfumo uliowekwa."

Alisema shirikisho hilo linafuata kanuni yake ya kutokuwa na upendeleo wa kidini au kisiasa wakati wa mechi.

Hii si mara ya kwanza FFF kuzua utata. Mwaka jana, marefa waliamriwa wasisimamishe mechi wakati wa magharibi ili wachezaji wanaofunga waweze kufuturu. Hii ilitofautiana na ligi kama Premier League ya Uingereza na Bundesliga ya Ujerumani, ambazo ziliwaruhusu wachezaji kufuturu.

Mashabiki wa PSG hata walishikilia bango lililosomeka:
"Tende moja, glasi ya maji, ndoto mbaya ya FFF."

Kwa mujibu wa shirikisho la soka la Ufaransa, mechi zinazositishwa ili kuruhusu wachezaji kufuturu hazikubaliki kwa mujibu wa katiba ya FFF.

"Dhana ni kwamba kila kitu kina wakati wake. Kuna wakati wa kucheza michezo, na kuna wakati wa kutekeleza ibada za dini," alisema Eric Borghini, rais wa Kamati ya Marefa wa Shirikisho, alipoongea na AFP.

Kwa mujibu wa Borghini, marufuku hii ni utekelezaji wa kanuni ya kwanza ya shirikisho inayotaka kuheshimu misingi ya "sekulari" katika soka.

Mbali na marufuku ya kufunga, FFF pia inazuia wachezaji wa kike kuvaa hijabu, hata baada ya FIFA kuondoa marufuku yake yenyewe.

Shinikizo la kuchukua hatua linaongezeka. Podcast ya "Everything Is Futbol" imewataka wachezaji Waislamu kususia timu ya taifa ya Ufaransa, ikisema:
"Utaona jinsi Ufaransa itakavyobadilika haraka mara watakapogundua hawawezi kuwa na timu bora bila wachezaji wengi wenye uraia pacha wa Ufaransa na Afrika."

3492145

captcha