Arbaeen ni tukio muhimu miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Shia, likiwa ni ukumbusho wa siku 40 za maombolezo baada ya Ashura ambayo ni siku ya kumkumbuka Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), aliyeuawa shahidi huko Karbala. Maelfu ya wafanyaziyara husafiri kuelekea Iraq, wakipitia miji ya Iran kama Qom, amba nim ji muhimu wa kidini.
“Qom ndiyo mji wa kwanza wa Iran kuandaa maadhimisho makubwa ya Arbaeen,” alisema Mehdi Ghorbanikaram, mkuu wa Kamati ya Arbaeen ya Umma ya Qom. “Ni msingi wa harakati ya Arbaeen katika ardhi ya Iran.”
Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 2,500 wanatarajiwa kutoa huduma moja kwa moja, huku wengine wakisaidia kwa njia zisizo za moja kwa moja. Kamati ina vitengo 22 vinavyoshughulikia masuala ya kimataifa, utawala, wanawake, wanaume na mahusiano ya umma.
Takriban nyumba 200 na shule 40 zimetengwa kwa ajili ya malazi. Vituo 1,000 vya Bayt al-Hussein pia vimeandaliwa. Hivi ni vituo vya ukarimu vya jamii vinavyofunguliwa wakati wa Arbaeen. Wafanyaziyara watahudumiwa bure: malazi, milo mitatu moto kwa siku, na huduma za afya.
Gharama za huduma za afya mwaka jana zilikadiriwa kufikia riali bilioni 70 (takriban dola 130,000). Ghorbanikaram alisisitiza umuhimu wa kuonesha utambulisho wa kiroho na kitamaduni wa Qom kwa wageni kutoka nje. “Kila mhujaji asiyekuwa Muirani ni balozi wa utamaduni wa Kiislamu anaporudi nyumbani.”
Pakistan iliongoza idadi ya mahujaji wa kimataifa, ikifuatiwa na Afghanistan, India, na Nigeria. Kwa ujumla, wafanyaziyara kutoka nchi 32 walitembelea Qom ndani ya miaka miwili iliyopita.
Hujjatul Islam Safar Fallahi, mkurugenzi wa haram ya Hazrat Masoumeh (SA), alithibitisha kwamba haram iko tayari kikamilifu kwa ujio wa mahujaji. Usambazaji wa vyakula, huduma za chai, na msaada wa afya kutoka Red Crescent na kliniki umepangwa. Shughuli za kitamaduni zitafanyika kwa kuzingatia usalama na utulivu wa wageni.
Arbaeen ya mwaka huu itakuwa tarehe 14 Agosti, huku huduma zikiendelea hadi mwisho wa mwezi wa Safar (24 Agosti) na huenda zikaongezwa hadi tarehe 5 Rabi al-Awwal (29 Agosti)
3494026