Akizungumza katika kikao cha ngazi ya juu na maafisa wa Idara ya Mahakama wa Iran jijini Tehran leo Jumatano, Ayatullah Khamenei amesema makabiliano hayo yalifichua sio tu nguvu za kijeshi na kistratijia za Iran, bali pia uthabiti, mwamko na umoja wa kitaifa wa watu wa Iran.
"Mafanikio makubwa ya watu (wa Iran) wakati wa vita vya siku 12 yalikuwa dhamira yao, nia, na kujiamini kwa taifa, kwa sababu kiini hasa cha kuwa na roho na utayari wa kukabiliana na nguvu kama Marekani na mbwa wake aliyefungwa, yaani utawala wa Kizayuni, ni muhimu sana," amesema Ayatullah Khamenei.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mabadiliko ya Iran kutoka kuwa mteja mtiifu chini ya utawala wa zamani wa Pahlavi hadi kuwa taifa lenye msimamo na huru.
"Huko nyuma, hata kwa faragha, maafisa (wa Iran) hawakuthubutu kuikosoa Marekani. Leo hii, Iran imefikia hatua ambayo sio tu haiiogopi Marekani lakini pia inaitia hofu na wahaka. "Moyo na utashi huu wa kitaifa ndio hasa unaoifanya Iran kujivunia na kuelekea katika barabara ya kufikia matarajio yake makubwa," amesema Kiongozi Muadhamu.
Ayatullah Ali Khamenei amewaambia maafisa wa mahakama wa Iran kuushtaki utawala wa Israel na mshirika wake Marekani kwa uvamizi wao wa hivi karibuni dhidi ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, wananchi wa Iran walikwamisha mahesabu na malengo ya wavamizi na kusisitiza kuwa, hivi sasa ni jukumu la kila mmoja kuhifadhi mshikamano huo wa kitaifa.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Iran kamwe haitaingia katika medani yoyote—kidiplomasia au kijeshi—kama upande ulio dhaifu zaidi. Kiongozi Muadhamu amesema hayo akiwahutubu viongozi wa nchi za Magharibi ambao kimakosa wanaamini kuwa uchokozi wa hivi karibuni umewapa fursa ya kuishinikiza Iran kidiplomasia.
"Tuna vifaa vyote muhimu kama vile akili na nguvu za kijeshi; kwa hivyo, iwe kwenye uwanja wa kidiplomasia au uwanja wa vita, kila tunaposhiriki, kwa neema ya Allah, tutaingia kwa mikono kamili," amesema Kiongozi Muadhamu, ambapo ameutaja wito wa Israel wa kutaka kusimamishwa vita baada ya siku 12 za uchokozi kuwa ni ushahidi wa wazi wa jibu kali la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni.
"Lau utawala wa Kizayuni ungelikuwa na uwezo wa kujilinda, usingeigeukia Marekani namna hiyo. Lakini ulielewa kuwa hauwezi kusimama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu."
Mnamo tarehe 13 Juni, utawala wa Kizayuni ulianzisha shambulizi la wazi na la kichokozi dhidi ya Iran, likiwalenga makamanda wa juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida.
Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani iliingia vitani kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran kwa mabomu.
Kama jibu la kulipiza kisasi, Jeshi la Iran lililenga maeneo ya kimkakati katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kituo cha kijeshi cha al-Udeid kilichoko Qatar, ambacho ndicho kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika eneo la Asia ya Magharibi.
3493876