Maelfu ya watu walimiminika barabarani na mitaani katika mji mkuu Sana'a baada ya Swala ya Ijumaa hapo jana, kushiriki maandamano hayo ya kitaifa, wakitangaza uungaji mkono wao usioyumba kwa Wapalestina wa Gaza, na kulaani mauaji ya kimbari ya Israel katika eneo hilo lililozingirwa.
Washiriki wa maandamano hayo walibeba mabango yenye jumbe za kulaani jinai za Israel, huku wakipiga nara tofauti kama "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel."
Wakati huo huo, wananchi wa Yemen katika mji wa Saada pamoja na miji mingine ya nchi hiyo, jana pia walifanya maandamano makubwa ya kuiunga mkono Palestina sanjari na kulaani vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji walitangaza kuunga mkono Wapalestina huko Gaza, huku wakilaani na kukosoa uhalifu wa kivita wa Israel kwa ushirikiano wa Marekani huko Gaza na katika miji mbali mbali ya Yemen. Aidha walipeperusha bendera za Palestina na kubeba picha za watoto waliouawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 58,000 wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.
3493895