IQNA

Papa Leo XIV alaani ‘Unyama’ wa Mashambulizi ya Israeli na mzingiro wa Gaza

20:42 - July 21, 2025
Habari ID: 3480975
IQNA – Papa Leo XIV amelaani vikali vita vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel Gaza, akielezea vita hiyo kuwa ya “kinyama” na kukosoa matumizi holela ya nguvu, huku makumi ya Wapalestina wakiripotiwa kuuawa wakiwa kwenye foleni ya msaada wa chakula.

Katika hotuba yake ya Jumapili wakati wa ibada ya Angelus huko Castel Gandolfo, Papa alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa “unyama wa vita” na kuhimiza suluhisho la amani kwa mgogoro huo.

Tukio hilo lilitokea wakati shirika la ulinzi wa raia la Gaza liliporipoti kuwa angalau Wapalestina 93 waliuawa kwa risasi za Israeli walipokuwa wakisubiri msaada wa chakula karibu na kivuko cha Zikim kaskazini mwa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, waliouawa walikuwa wakisubiri msaada kutoka kwa malori ya Umoja wa Mataifa waliposhambuliwa kwa risasi. Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya raia waliokuwa wakitafuta misaada ya kibinadamu.

Katika maeneo mengine ya ukanda huo, msemaji wa ulinzi wa raia Mahmud Basal aliripoti kuwa watu tisa waliuawa kwa risasi karibu na kituo cha usambazaji wa msaada huko Rafah, na wengine wanne waliuawa katika tukio kama hilo huko Khan Younis. Mashambulizi haya yalitokea ndani ya siku moja kufuatia vifo vya awali katika maeneo hayo hayo.

Jeshi la Israeli lilikiri kufyatua risasi kwa kundi kubwa la watu kaskazini mwa Gaza, likidai kuwa kundi hilo lilikuwa tishio kwa wanajeshi wake.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa msafara wa malori 25 ya msaada wa chakula ulikutana na “umati mkubwa wa raia wenye njaa” karibu na Jiji la Gaza. WFP ilieleza kuwa msafara huo ulipigwa risasi, na kuongeza: “WFP inasisitiza kuwa aina yoyote ya vurugu dhidi ya raia wanaotafuta msaada wa kibinadamu haikubaliki kabisa.”

Daktari Mohammed Abu Salmiya, mkurugenzi wa Hospitali ya al-Shifa, aliiambia shirika la Associated Press kuwa miili 48 na majeruhi zaidi ya 150 walifikishwa hospitalini kutoka eneo la Zikim. Alisema bado haijafahamika wazi kama mashambulizi hayo yalifanywa na jeshi la Israeli, makundi yenye silaha, au wote kwa pamoja.

 Papa Leo XIV pia alieleza huzuni yake kuhusu shambulizi la Israel dhidi ya kanisa pekee la Wakatoliki Gaza, ambalo liliua watu watatu na kuwajeruhi wengine 10, akiwemo padri wa parokia hiyo ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Papa Francis wa zamani.

“Kitendo hiki, kwa masikitiko, kinaongeza kwenye mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea dhidi ya raia na maeneo ya ibada Gaza,” alisema Papa.

Aliendelea kutoa wito kwa viongozi wa dunia, akiwataka “kuzingatia sheria za kibinadamu za kimataifa na kuheshimu wajibu wa kuwalinda raia, pamoja na marufuku ya adhabu ya pamoja, matumizi holela ya nguvu, na kuhamishwa kwa nguvu kwa watu.”

Tangu vita hiyo ianze tarehe 7 Oktoba 2023, angalau Wapalestina 58,895 — wengi wao wakiwa wanawake na watoto — wameuawa, huku zaidi ya 140,000 wakijeruhiwa.

3493925

captcha