IQNA

Ukombozi wa Palestina

Taarifa ya Hamas kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds

18:43 - April 14, 2023
Habari ID: 3476867
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetoa taarifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kutaka kuweko harakati ya kimataifa ili kuunga mkono muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina na kuhitimisha uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.

Harakati ya Hamas imetangaza katika taarifa yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds kwamba, kukombolewa Quds na Msikiti wa Al-Aqsa ni jukumu la Wapalestina wote na Umma mzima wa Kiislamu.

Hamas imeongeza katika taarifa hiyo kwamba, Siku ya Quds ni hafla ya kuukumbusha Umma wa Kiislamu na watu wote walio huru duniani kuhusu wajibu wao katika kutetea na kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa na Al-Quds, ambavyo vinakabiliwa na ongezeko la mashambulizi na hujuma tangu ardhi ya Palestina ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu.

Taarifa ya Hamas imeeleza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa ya kuunganisha juhudi za Umma katika kuunga mkono mapambano ya wakazi wa Quds, na imepongeza misimamo ya nchi zote na Umma wa Kiislamu na Kiarabu na vilevile watu huru ya kuendelea kutetea haki za taifa la Palestina na mapambano yake halali.

Hamas imesisitiza katika taarifa hiyo kwamba, mji wa Quds na Msikiti wa Al-Aqsa ndio kitovu cha mgogoro na adui Mzayuni; Adui anayeikalia kwa mabavu Palestina, anawaua kwa umati watu wa ardhi hiyo na kuwafukuza kutoka katika nchi yao na kutaka kuyayahudisha maeneo matakatifu.

Harakati ya Hamas imesema kuwa, Al-Quds na Msikiti wa Al-Aqsa zinasalia kuwa moyo unaodunda wa Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu na ni nembo ya watu wote walio huru duniani. Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa, ni jukumu la watu wa matabaka yote na Umma wa Kiislamu kuikomboa Al-Quds na Msikiti wa Al-Aqsa kutoka kwenye makucha ya fashisti mtendajinai. 

Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa: "Tunatoa ahadi kwa taifa la Palestina ndani na nje ya nchi na katika kambi za wakimbizi wanaoendelea kutoa mhanga maisha yao kwa ajili ya kutetea ardhi, Quds na wafungwa wa Kipalestina, kwamba tutarejesha haki zao halali na kukidhi matakwa ya kuunda taifa uhuru ambalo mji mkuu wake utakuwa Quds Tukufu."

4133973

Habari zinazohusiana
captcha