IQNA

Rais wa Iran

Taifa la Iran litashiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds

12:02 - April 13, 2023
Habari ID: 3476859
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi amesema: taifa adhimu la Iran litatangaza kwa mara nyingine tena kwamba litabaki kuwa thabiti katika malengo ya Uislamu hadi itakapokombolewa Quds kikamilifu, kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds.
Ijumaa ya tarehe 14 Aprili itakayosadifiana na tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Quds Duniani.
 
Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Quds kwa ubunifu wa Imam Khomeini (MA), mwasisi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amehutubia hadhara ya waumini katika Haram ya Imam Khomeini (MA) kwa mnasaba wa mkesha wa tarehe 21 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani iliyosadifiana na kumbukumbu ya kufa shahidi kiongozi wa wachamungu Amirul-Mu'minin Ali (AS), ambapo katika hotuba yake hiyo amesema, Imam Khomeini alilitangaza suala la Quds na Palestina kuwa kadhia muhimu zaidi kwa Ulimwengu wa Kiislamu na akaifanya Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds na Siku ya kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa. Rais Raisi amesisitiza kwa kusema: "bila shaka yoyote katika siku ya 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani itakayosadifiana na Siku ya Quds Duniani, taifa adhimu la Iran litashiriki kwa wingi katika maandamano na kutangaza kwamba litabaki kuwa thabiti katika malengo ya Uislamu hadi Quds itakapokombolewa kikamilifu".

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "leo hii, ambapo mfumo wa ubeberu duniani unafuatilia kueneza chuki dhidi ya Iran, chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya Ushia, sisi sote, -wakiwemo viongozi, wanafunzi wa dini, mashekhe, maulamaa, makhatibu, wahadhiri wa vyuo vikuu na wale wenye fursa za kutumia vyombo vya habari-, tuna wajibu wa kuzungumza na vijana na kutekeleza Jihadi ya Ubainishaji ili kuondoa utata walionao akilini mwao".

4133533

captcha