IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Kikao cha nchi za Kiarabu na Kiislamu cha Riyadh kuhusu Gaza chamalizika kwa maamuzi muhimu kadhaa

21:08 - November 11, 2023
Habari ID: 3477877
TEHRAN (IQNA)- Kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kilichofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia kimetilia mkazo ulazima wa kuondolewa mzingiro dhidi ya Gaza na kuingia misafara ya misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Kikao cha pamoja cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilifanyika leo mjini Riyadh kwa lengo la kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu.
 
Katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo, viongozi wa nchi washiriki wamelaani mashambulizi ya utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na uhalifu wa kivita na mauaji ya kutisha uliyofanya, na wametilia mkazo ulazima wa kuondolewa mzingiro iliowekewa Gaza na kutumwa haraka misaada ya kibinadamu katika eneo hilo ikijumuisha bidhaa za chakula, dawa na mafuta.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: "tunalitaka Baraza la Usalama lichukue uamuzi wa haraka kulaani uharibifu wa kinyama uliofanywa na Israel katika hospitali za Ukanda wa Gaza. Aidha tunazitaka nchi zote ziache kuwapelekea silaha na zana za kivita viongozi wa utawala ghasibu."

Taarifa ya mwisho ya kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu imesisitiza pia kwamba hata vikihalalishwa kwa kisingizio chochote kile, inapinga maelezo ya kuviita vita vya ulipizaji kisasi dhidi ya Gaza kuwa ni hatua ya kujilinda.

Washiriki wa mkutano wa wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu wamesisitiza pia katika taarifa ya mwisho ya mkutano wao kwa kusema: "tunalaani hatua ya kutaka kuwahamisha Wapalestina wapatao milioni moja na nusu kutoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka kusini, ambayo inachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita kulingana na Mkataba wa Nne wa Geneva wa 1949 na kiambatisho chake cha mwaka 1977. Na tunazitaka pande zinazohusika na makubaliano ya Geneva zichukue maamuzi na hatua za pamoja katika kuulaani hatua hiyo, na pia tunazitaka taasisi zote zinazohusika za Umoja wa Mataifa kukabiliana na njama za viongozi wa utawala ghasibu za kuendeleza hali hii ya kusikitisha na isiyo ya kibinadamu na kutilia mkazo haja ya kurejea haraka wakimbizi wa Kipalestina kwenye makazi na maeneo yao".

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa kuwahamisha kwa nguvu, kuwabaidisha au kuwalazimisha Wapalestina waondoke kwenye maeneo yao iwe ni ndani ya Ukanda wa Gaza au Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwa ni pamoja na Baitul Muqaddas, au nje ya eneo hilo na kuwapeleka mahali pengine popote ni mstari mwekundu na ni uhalifu wa kivita.

/4181174

Kishikizo: gaza oic
captcha