IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Rais wa Iran: Vita vya Gaza ni makabiliano kati ya mhimili wa heshima na mhimili wa uovu

21:37 - November 11, 2023
Habari ID: 3477878
RIYADH (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika kikao cha pamoja cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwamba: kadhia ya Gaza ni makabiliano baina ya mhimili wa sharafu au heshima na mhimili wa uovu, na kila mtu anapaswa abainishe yuko upande gani.
Akihutubia kikao hicho kilichofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia, Sayyid Ebrahim Rais ameitaja serikali ya Marekani kuwa ni muamrishaji na mshirika mkuu wa jinai zilizofanywa na Wazayuni katika wiki tano zilizopita dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza na akasema: inapasa hivi sasa tushike hatamu za masuala bada ya jumuiya za kimataifa kupoteza utambulisho, kushindwa kuchukua maamuzi na kuwa na hali isiyoeleweka kutokana na kuwekwa chini ya satua na ushawishi wa Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amependekeza katika kikao hicho hatua kumi zinazopasa kuchukuliwa kwa haraka za maamuzi madhubuti yenye manufaa kwa taifa la Palestina, ikiwa ni pamoja na "kusimamishwa mauaji ya watu wa Gaza", "kuondolewa kikamilifu mzingiro wa kibinadamu wa Gaza", "kuondoka kijeshi haraka utawala wa Kizayuni katika eneo hilo", "kukata nchi za Kiislamu mahusiano yote ya kisiasa na kiuchumi na utawala wa Kizayuni", "kuanzishwa mahakama ya kimataifa ya kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu viongozi wahalifu wa Kizayuni na Marekani", "kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya ujenzi mpya wa haraka wa Gaza utakaogharimiwa na nchi za Kiislamu" na "kutumwa na nchi za Kiislamu msafara wa meli za misaada za kibinadamu kwa watu wa Palestina".

Rais Raisi ametamka kinagaubaga kuwa Israel ni mwana wa haramu wa Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Iran amebainisha kuwa, Marekani iliuhamasisha na kuushajiisha utawala wa Kizayuni kutekeleza operesheni za kinyama na jinai dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza baada ya kuunda haraka baraza lake la mawaziri la kijeshi.

Sayyid Raisi ameendelea kueleza kwamba: sambamba na hayo, meli za kivita za Marekani zilitumwa katika eneo; na kwa kufanya hivyo Washington ikawa imeingia vitani kivitendo kwa manufaa ya Israel. Aidha, kutoa uungaji mkono wa pande zote kwa utawala wa Kizayuni katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuzuia kupitishwa azimio la kukomesha mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Gaza ni huduma nyingine iliyotoa Marekani kwa wavamizi ili kuwapa fursa kamili ya kutenda uhalifu mkubwa zaidi wa kivita kuliko uliowahi kufanya wakati wowote ule.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kwamba ufisadi na uharibifu wote unaongozwa na Marekani, ikiwa ni pamoja na mauaji ya mamilioni ya watu duniani, kuanzia Afghanistan, Iraq, Syria na nchi nyingine za Kiislamu.

4181182
Habari zinazohusiana
captcha