Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imelaani vikali vitendo vya hivi karibuni vya Wazayuni, vikiwemo vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu na kuvunjiwa heshima misikiti ya Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake, Jumuiya hiyo pia ilieleza kuunga mkono jibu la awali la Hizbullah kwa chokochoko hizo na kusifu operesheni za baharini za jeshi la Yemen.
Jumuiya hiyo ilikosoa hali ya kutojali ya baadhi ya serikali za Waarabu na Waislamu, wananchi na wanazuoni dhidi ya ukatili unaoendelea Palestina, yakiwemo mauaji ya halaiki, mauaji ya kimbari na mauaji ya kila siku.
Imeashiria nafasi ya taasisi ya Kizayuni katika jinai hizo na uungaji mkono unaopata kutoka Marekani na nchi nyingine za Magharibi.
Jumuiya hiyo ilitambua juhudi za wale wanaosimama na Gaza, ikiwa ni pamoja na Hizbullah na jeshi la Yemen, na kutoa wito kwa watu wote, serikali, na wasomi kuondokana na uzembe wao na kutekeleza kikamilifu majukumu yao katika kukabiliana na dhulma hizi.
Picha zilizotolewa Ijumaa iliyopita zilionyesha wanajeshi wakichoma nakala za Qur'ani Tukufu katika msikiti mmoja katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
Kituo cha habari cha Qatar cha Al Jazeera kimesema kimepata picha hizo kutoka kwenye video iliyochukuliwa na wanajeshi wa Israel na ndege zisizo na rubani ambazo zilipatikana Gaza.
Picha hizo zilionyesha wanajeshi wa Israel wakivamia Msikiti wa Bani Saleh ulioko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kisha kurarua na kuchoma nakala za Quran ndani ya msikiti huo.
Katika picha zaidi, jeshi la Israel linaonyeshwa likiharibu Msikiti Mkuu huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, ambao ni moja ya misikiti mikongwe zaidi huko Gaza, uliojengwa miaka 96 iliyopita.
Kuharibu au kuinajisi Quran ni kosa kubwa chini ya Uislamu na ni tusi kwa imani ya Waislamu wapatao bilioni 1.9 duniani kote.
Katika kipindi cha mashambulizi ya miezi 10 ya utawala wa Israel huko Ghaza, mamia ya misikiti ukiwemo Msikiti Mkuu wa Omari uliojengwa eneo la Mji wa Gaza yapata miaka 1,000, imeharibiwa kwa kiasi au kabisa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali iliyoko Gaza, jeshi la Israel limeharibu kabisa misikiti 609 na pia kuharibu makanisa matatu kote Gaza tangu Oktoba 7, kuanza kwa vita dhidi ya Gaza.
Tangu Israel ianze kampeni yake dhidi ya Gaza miezi 10 iliyopita, makumi ya nchi na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yameshutumu ulipuaji wa hospitali, makazi ya raia, na nyumba za ibada - yote hayana kikomo kwa mashambulizi chini ya sheria za vita.
Zaidi ya Wapalestina 40,300 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa katika mashambulizi hayo ya Israel.
3489646