IQNA

Taazia

Wairani washiriki mazishi ya pamoja ya wahanga wa ugaidi Kerman

21:26 - January 05, 2024
Habari ID: 3478151
IQNA-Wananchi wa Iran leo Ijumaa wamefanya shughuli ya mazishi ya pamoja kwa wahanga wa miripuko miwili ya kigaidi iliyotokea Jumatano katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa nchi huku kamanda wa ngazi ya juu wa Iran akiahidi kuwasaka magaidi popote walipo.

Maelfu ya wananchi wa Iran pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali akiwemo Rais Ebrahim Raisi wameshiriki katika shughuli ya mazishi katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran. 

Shambulio la kigaidi lililotekelezwa juzi Jumatano huko Kerman limeua shahidi watu wasiopungua 84 na kujeruhi wengine 285. Hujuma hiyo ya kigaidi ilitekelezwa katika kumbukumbu ya  kumuenzi Kamanda wa vita dhidi ya ugaidi Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyeuliwa kigaidi na Marekani huko Baghdad Iraq miaka minne iliyopita.

Mbali na Kerman, miji mingine ya Iran leo imeshuhudia maandamano ya wananchi baada ya Sala ya Ijumaa ya kulaani mashambulizi ya kigaidi ya Kerman na waungaji mkono wake. Wafanya maandamano walikuwa wakipiga nara dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. 

Rais wa Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hakuna uungaji mkono au msaada wowote kutoka nchi yoyote utakaowaacha salama vibaraka waliohusika katika jinai ya kigaidi huko Kerman.

Nchi mbalimbali zimelaani jinai hiyo ya kigaidi huko Kerman; ambapo jana Alhamisi Rais  Aleksandar Vučić wa Serbia alizungumza kwa simu na Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kulaani hujuma hiyo ya kigaidi. Rais wa Serbia ametoa mkono wa taazia na pole kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema: Anataraji kuwa wahusika wa jinai hiyo watafakishwa mahakamani haraka iwezekanavyo. 

Katika mazungumzo hayo na Rais wa Serbia, Rais Ebrahim Raisi pia amesisitiza kuhusu kuadhibiwa vikali wapangaji na watekekezaji wa jinai hiyo ya kigaidi, na kueleza kuwa vitendo hivyo vya woga havitazuia taifa kubwa la Iran kuachana na malengo yake makuu ya kupambana na dhulma, uistikbari na ukandamizaji. Amesema, hakuna uungaji mkono au msaada wowote kutoka nchi yoyote utakaowaacha salama vibaraka waliohusika katika jinai ya kigaidi huko Kerman. 

Leo Ijumaa Raisi Raisi ameelekea Kerman ili kushiriki katika mazishi ya mashahidi wa jinai hiyo ya kigaidi; ambapo baada ya kulizuru kaburi la Shahidi Qassim Soleimani, amewatembelea majeruhi wa jinai ya juzi ya kigaidi na kufahamishwa kuhusu utaratibu wa kuwapatia matibabu. 

Kamanda wa IRGC

Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wananchi huko Kerman, Meja Jenerali Hossein Salami Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema: Wanachama wa kundi la kigaidi waliohusika katika milipuko ya karibuni katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran watatambuliwa na kufikishwa mahakamani popote walipo.

Kamanda Salami amelitaja kundi la Daesh kuwa ni zao la sera za Marekani katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Kundi hilo la kigaidi lilitaka kuchora ramani mpya, na  kuanzisha utawala wa Khilafa katika ulimwengu wa Kiislamu lakini lilishindwa kutokana na kujitolea kwa Jenerali Soleimani. "Daesh wametoweka na hakuna alama yoyote yao kwenye ramani ya kisiasa ya dunia na wamepotea na kujificha kwenye vibanda",amesema Meja Jenerali Hossein Salami. 

Kundi la kigaidi la Daesh au ISIS limedai kuhusika na milipuko miwili iliyoua watu 84 na kujeruhi wengine wengi katika kumbukumbu ya kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran.

Katika taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Telegram, kundi hilo la kigaidi limesema wanachama wake wawili walilipua mikanda yao ya vilipuzi katika umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kwenye makaburi kwa ajili ya kumbukumbu ya mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Jenerali Soleimani.

 

3486687

captcha