Akizungumza katika hafla mjini Tehran siku ya Alhamisi ya kuadhimisha miaka mitano ya kuuawa shahidi kwa Jenerali Soleimani Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: "Tutasimama kwa ajili ya ukweli na kuendelea na njia hii kwa nguvu." Aidha amesema Iran itawadhlilisha waliomuua shahidi Jenerali Soleimani.
Halikadhalika amesema: "Tunaahidi kwamba tutaendelea na njia ya Shahidi Soleimani kwa nguvu na kusimama dhidi ya dhulma maadamu tupo hai."
Rais alisema kwamba Jenerali Soleimani alifedhehesha madhalimu kwa damu yake. Amebanisha zaidi kwa kusema: "Mtu kama huyo alipaswa kuuawa shahidi na kuonyesha kwamba Marekani, Israel na Ulaya, wanaodai kwa uwongo kuunga mkono ubinadamu na haki za binadamu, ni waongo.
Rais wa Iran ameongeza kwamba: "Wao kwa hakika ni maadui wa ubinadamu. Unaweza kuona walivyo wanyama na jinai wanazofanya."
Rais Pezeshkian amesema kwamba lengo kuu na jitihada za Jenerali Soleimani zilikuwa ni kuleta umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Kwa mujibu wa rais, kamanda huyo hakujali mchana wala usiku popote alipohitajika kuwatetea wanyonge bila kujali dini yao, iwe ni Iraq, Syria, Lebanon, Afghanistan, au sehemu nyingine yoyote.
Rais aligusia juhudi za maadui za kuzusha mgawanyiko nchini Iran kwa msaada wa baadhi ya watu wanaopinga mapinduzi na wanaolenga kutekeleza njama zao nchini.
Amesema: "Lazima tujitahidi kuhakikisha kwamba njama zao na mipango yao miovu haifanikiwi, na hili litawezekana kwa msaada wa Wairani wote wapendwa."
Pezeshkian aidha amesema hatua ya kwanza ya umoja ni kutii na kuunga mkono sera za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, na kisha kushughulikia matatizo ya watu wa Iran.
Jenerali Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji cha Iraq (PMU) na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani Januari 3, 2020 karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Shambulizi hilo la kigaidi liliidhinishwa na Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Makamanda hao wawili walikuwa wakiheshimika sana katika eneo la Asia Magharibi na duniani kote kwa sababu ya jukumu lao muhimu katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh katika eneo hilo hususan Iraq na Syria.
4257738